Iringa. Kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Chanel ten, Daudi Mwangosi inayomkabili askari polisi, Pacificus Cleophace, jana ilianza kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Iringa chini ya Jaji Paulo Kihwelo kwa shahidi wa kwanza kuelezea namna walivyotekeleza agizo la aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Shahidi huyo ambaye ni ofisa mstaafu wa Jeshi la
Polisi katika Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Saidi Mnunka (61) alidai
kuwa kabla ya tukio Septemba Mosi, mwaka 2012 alipata maelekezo kutoka
kwa Kamanda Kamuhanda kuwa apange seksheni kwa ajili ya kuzuia ghasia
siku inayofuata katika mkutano wa Chadema uliopangwa katika Kijiji cha
Nyololo wilayani Mufindi.
Alisema seksheni hiyo ilikuwa na askari 12
aliowapatia maelekezo aliyopewa na Kamuhanda na aliwaamuru wachukue
silaha kwa ajili ya kuelekea katika eneo la tukio.
Silaha walizochukua ni pamoja na mabomu ya machozi, virungu, mabomu ya mshindo na silaha za moto mbili.
Alisema wakati huo pia Serikali ilikuwa imetoa
katazo kwa vyama vyote vya siasa kutofanya mikutano ya hadhara ili
kupisha kazi ya sensa ya watu na makazi iliyokuwa ikiendelea nchini.
Alidai kutokana na tamko hilo, Chadema walipatiwa barua kutoka makao
makuu ya Polisi Mkoa wa Iringa iliyowataka wasitishe maandamano na
mkutano wao wa hadhara kama walivyokuwa wameomba.
Hata hivyo, alidai kuwa wafuasi na viongozi wa
chama hicho walikiuka agizo la Polisi na kuamua kufanya maandamano na
mkutano na walipoamriwa kutawanyika walikaidi na kuamua kuanzisha
vurugu.
“Nilichokishuhudia siku ile niliona kikosi cha askari kikiwa kimemzunguka mwandishi wa habari huku wakimpiga, ndipo Kamanda Kamuhanda akaagiza waache kumpiga kwa kuwa alikuwa ni mwandishi, lakini kabla agizo hilo halijatekelezwa nilisikia kishindo kikubwa na nikauona mwili wa marehemu Daudi Mwangosi ukiwa umelala chini huku utumbo ukiwa nje na askari wengine wakiwa hapo chini wamejeruhiwa,” alisimulia shahidi huyo.
“Nilichokishuhudia siku ile niliona kikosi cha askari kikiwa kimemzunguka mwandishi wa habari huku wakimpiga, ndipo Kamanda Kamuhanda akaagiza waache kumpiga kwa kuwa alikuwa ni mwandishi, lakini kabla agizo hilo halijatekelezwa nilisikia kishindo kikubwa na nikauona mwili wa marehemu Daudi Mwangosi ukiwa umelala chini huku utumbo ukiwa nje na askari wengine wakiwa hapo chini wamejeruhiwa,” alisimulia shahidi huyo.
Kwa upande wake Wakili wa Serikali, Sunday Ihela
aliiomba mahakama hiyo ipokee gazeti la Mwananchi la Septemba 3, mwaka
2012 kama kielelezo kutokana na picha iliyokuwa imechapishwa kuhusiana
na mauaji hayo.
Jaji Kihwelo aliiahirisha kesi ambayo inaendelea
kusikilizwa leo baada ya Wakili wa upande wa utetezi, Rwezaula Kaijage
kupinga kupokelewa kwa kielelezo hicho akitaka mwandishi wa habari hiyo
ahojiwe kwanza.
No comments:
Post a Comment