Monday, 15 June 2015

ACT KUTANGAZA MGOMBEA KITI CHA URAIS MWEZI WA NANE ...



Chama cha ACT - Wazalendo kinatarajia kumtagaza mgombea wake wa urais wa Agosti 10, imefahamika.

Chama hicho kimesema mtia nia atakayepeperusha bendera ya ACT - Wazalendo atawajibika kutangaza mali binafsi na vyanzo vyake kwa kufuata utaratibu ulioanishwa katika katiba ya chama hicho.

Hayo yalisemwa jana mjini Geita na Kiongozi wa Chama hicho, Zitto Kabwe wakati akihutubia mamia ya wananchi katika viwanja vya Stand mjini hapa.

      

Alisema Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho iliyokutana juzi mjini Tabora, imepitisha ratiba kamili ya kuchukua na kurudisha fomu kwa nafasi mbalimbali za chama hicho kuanzia Julai Mosi.

“Kuanzia Julai Mosi mpaka Julai 17 ni kuchukua fomu kwa ngazi ya udiwani kwa ada ya Sh10,000, Julai 1-26 kuchukua fomu kwa ngazi ya ubunge na uwakilishi na ada yake ni Sh20,000 na kwa ngazi ya urais shughuli hiyo itakuwa kati ya Julai 1-26 na ada yake ni Sh100,000,” alisema Zitto na kuongeza:
“Vikao vya ngazi mbalimbali ya uteuzi vitaanza kuanzia Julai 27 hadi Agosti 10 mkutano mkuu wa chama utakapopitisha jina la mgombea urais.”

Sifa za mgombea urais

Zitto alisema lazima mgombea huyo awe amethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT - Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi, awe ni mtu anayejitegemea kutokana na chanzo halali cha kipato kutokana na shughuli halali.

Alisema pia atakayetaka kukiwakilisha chama hicho kwa nafasi ya urais, itampasa kuwa mwenye haiba na taswira ya kuiwakilisha na kuipa heshima stahiki Tanzania katika Jumuiya za Kimataifa.
Chama hicho kinaendelea na ziara yake ya kulinadi azimio la Tabora lililozinduliwa juzi Mjini Tabora likilenga kuhuisha Azimio la Arusha. Leo watakuwa katika Mkoa wa Kagera.

No comments:

Post a Comment