Kazi ya uandikishaji wapigakura imezidi kukumbwa na matatizo baada ya wananchi kuwafgungia waandikishaji ndani ya kituo kutokana na kupata taarifa kuwa muda uliopangwa kwa ajili ya mitaa ya Buhalahala, Kisesa na Moringe umekwisha, huku wakiwa hawajapata nafasi ya kusajiliwa.
Wakati vurugu hizo zikitokea, wananchi wa kata nne
za wilayani Bukombe wanahofia kukosa nafasi ya kuandikishwa kutokana na
maeneo yao kutoingizwa kwenye mfumo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
huku watu watatu, wakiwamo watoto wawili wilayani Hanang wakikamatwa
kutokana na kujiandikisha mara mbili huku wakiwa hawajafikia umri
unaotakiwa.
Tukio la Geita limetokea siku chache baada ya
mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwataka wananchi mkoani
Kilimanjaro kutoruhusu mashine zinazotumika kuandikishia wapigakura kwa
njia ya kielektroniki (BVR) kuondolewa vituoni endapo kuna watu ambao
hawajaandikishwa.
Uandikishaji mkoani Geita ulianza Juni 17, mwaka
huu kwa kata tatu za Buhalahala, Mwatulole na Kalangalala na muda
uliopangwa kumalizika ni juzi. Hali ilikuwa mbaya kwenye kata hizo baada
ya wananchi kukaa vituoni hadi usiku wakisubiri kuandikishwa, na
walipopata taarifa kuwa kazi hiyo haitaendelea kwa kuwa siku
zilizopangwa zimemalizika, walichukua uamuzi huo wa kuzuia waandikishaji
hadi watakapoandikisha wote waliokuwa wamesalia.
“Nimekuja hapa nina siku ya tano leo (juzi). Kila
nikija sipati nafasi ya kuandikishwa wengine wanakesha vituoni siku ya
tano, lakini hawajaandikishwa na leo ndiyo mwisho,” alilalamika mkazi wa
Mwatulole, Marwa Ernest.
Mkazi mwingine, Neema Charles
alisema:“Mwandikishaji anatuambia macho hayaoni, kwa hiyo sisi
tufanyeje, tunataka kitambulisho kwani ndiyo cha msingi mwaka huu.”
Wananchi hao ambao walionekana kuwa na jazba, huku
wakitishia kuchoma mashine kama wasingeandikishwa, walidai kuwa
shughuli hiyo imetawaliwa na rushwa.
Hali hiyo ilikikumba kituo cha Shule ya Sekondari
ya Kalangalala, ambako hadi saa 1:30 usiku mwandishi alishuhudia zaidi
ya wananchi 200 wakiwa kituoni wengine wakipigana na kusukumana kila
mmoja akitaka kuandikishwa.
“Hapa muda unaisha na leo (juzi) ndiyo mwisho,
hatujui hatima yetu, wananchi wengi hatujaandikishwa, tumeshaomba
tuongezewe mashine lakini hatusikilizwi zaidi tunashuhudia wenye fedha
ndiyo
wanaandikishwa,” alisema mkazi wa Kisesa, Mariana Peter.
wanaandikishwa,” alisema mkazi wa Kisesa, Mariana Peter.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita,
Hellen Kahindi alikiri kuwapo kwa vurugu hizo na kwamba walikosea kuweka
vituo pembezoni mwa mji, jambo lililosababisha wananchi wa mjini
kukimbilia maeneo hayo wakihofia kutoandikishwa.
Alisema vurugu hizo zilisababisha magari mawili ya
Serikali kuvunjwa vioo, huku waandikishaji wakiponea chupuchupu
kutokana na kuwapo na vurugu kubwa eneo la kutokea hadi polisi
walipoingilia kati.
“Tunashukuru hakuna madhara makubwa yaliyotokea
kwa waandikishaji na vifaa, lakini tumejipanga kwa zoezi hili jipya ili
matatizo hayo yasijitokeze kwani tumeongeza wino na kwenye mashine,”
alisema Kahindi.
Wakati huohuo; wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita,
huenda wakashindwa kuandikishwa kutokana na kata zao nne kutowekwa
kwenye mfumo wa utawala na hivyo kutotambulika na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi, maofisa wa
kata hizo mpya za Katente, Katome, Bulangwa na Bulenga walisema maeneo
yao hayamo kwenye mfumo wa NEC.
Ofisa mtendaji Kata ya Katome, Lukuba Shitwala
alisema kutokana na kata yake kutokuwa kwenye mfumo huo, huenda zaidi ya
wananchi 9,000 wakakosa kuandikishwa.
Hata hivyo, mkurungenzi mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Bukombe, James Ihunyo alisema tayari kata hizo zimeingizwa
NEC, licha ya awali kutokuwamo, hivyo akawaomba watendaji kuhamasisha
wananchi kujitokeza vituoni.
Watoto wajiandikisha Hanang’
Watoto wawili wenye umri wa miaka 15 wa Kijiji cha
Nangwa, wilayani Hanang’ na mtu mwingine mmoja wilayani Babati mkoani
Manyara wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujiandikisha zaidi ya
mara tatu huku wakiwa hawajafikia umri wa 18 unaotakiwa.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Joel Bendera alisema
atahakikisha wote wanafikishwa mahakamani ili wachukuliwe hatua kali za
kisheria kwa kuwa alishapiga marufuku watu kujiandikisha zaidi ya mara
moja.
Mbali na watoto hao, mtu mwingine alijiandikisha
mara tatu ni mkazi wa Boay wilayani Babati aliyetumia majina tofauti,
akiitwa Petro Hhari kwenye kituo cha Shule ya Msingi ya Ditsoma A, Peter
Tluway katika kituo cha zahanati na Peter Hary katika kituo cha ofisi
ya kijiji hicho.
Mratibu wa BVR mkoani Manyara, Mwajabu Nyamkomola alithibitisha kupata taarifa za matukio hayo.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Mahamud Kambola alisema uandikishwaji unaendelea vizuri na wananchi wajitokeze.
No comments:
Post a Comment