Waziri wa ardhi nchini Kenya aliyesimamishwa kazi Charity Ngilu amefikishwa mahakamani na kujibu mashtaka ya kuwazuia maafisa wa shirika la kupambana na ufisadi kuchunguza stakabadhi za ardhi moja ambayo umiliki wake
una utata jijini Nairobi. Ngilu aliachiliwa kwa dhamana ya dola elfu kumi pesa tasilimu na ni waziri wa pili kushtakiwa baada ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuwataka maafisa wa umma wanaodaiwa kushiriki katika ufisadi kufunguliwa mashtaka.Ngilu ambaye alishtakiwa na watu wengine wanne alifika mahakamani saa tatu asubuhi lakini hakuhitajika kukiri ama kukanusha mashtaka kwa sababu mawakili wake walipinga kesi hiyo kuanza ilivyo wakitaka itenganishwe na ile ya washukiwa wengine.
Bi Ngilu anatuhumiwa kwa kuwazuia wapelelezi wa tume ya ufisadi nchini Kenya kwa kuagiza maafisa wa wizara ya ardhi kutowapa stakabadhi, rekodi ama taarifa yoyote kuhusina na ardhi hiyo yenye mzozo wa umiliki.
Upande wa mashtaka ulikataa kuyatenganisha mashtaka ya Ngilu na washukiwa wengine na hakimu akaagiza mawakili wa pande zote wakutane Ijumaa Ijayo kutoa mwelekeo kuhusu mkondo utakochukua kesi hiyo.
Kesi hiyo ilivutia umati mkubwa wa watu mahakamani akiwemo aliyekuwa makamu wa Rais wa Kenya Kalonzo musyoka na viongozi mbalimbali wa kisiasa.
Mbali na Ngilu aliyekuwa waziri wa uchukuzi Michael Kamau vile vile alishtakiwa kwa matumizi mabaya ya afisi na kukiuka kanuni za kutoa zabuni alipokuwa kihudumu kama katibu katika wizara hiyo.
Mwezi machi mwaka huu Rais Uhuru Kenyatta alitoa orodha ya maafisa mia175 wa serikali wakiwemo wabunge ambao alitaka tume ya kupambana na ufisadi ishirikiane na afisi na kiongozi wa mashtaka kuwachunguza na
kuwafungulia mashtaka kutokana na madai mbalimbali ya ufisadi yaliyokuwa yakiwakabili.
No comments:
Post a Comment