Afrika Kusini imesema kuwa huenda
ikajiondoa kutoka kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC
yenye makao yake makuu huko Hague Uholanzi kufuatia jaribio la kumkamata
rais wa Sudan Omar al Bashir alipokuwa nchini humo majuzi.
Lakini baada ya kikao maalum cha baraza la mawaziri nchini humo, serikali ilitoa onyo kuwa huenda ikalazimika kujiondoa kutoka kwa makubaliano yeyote na mahakama ya ICC kutokana na sababu kadha.
''Serikali inawajibu wake wa kimataifa lakini pia inawajibu wake kisiasa''taarifa hiyo ilisema.
''iwapo hatutakuwa na suluhisho maalum itakayotusaidia kutanzua taharuki iliyopo kwa sasa nafikiri serikali yetu haitakuwa na budi ila kujiondoa kutokana na makubaliano yeyote na ICC''iliendelea kusema.
Mahakama ya Afrika Kusini ilikuwa imemuagiza rais Bashir kusalia nchini humo huku ikijadiliana kuhusu iwapo agizo hilo la kukamatwa kwake litekelezwe au la.
Lakini kabla ya mahakama hiyo kutoa uamuzi wake rais Bashir aliondoka nchini Afrika Kusini na kurejea nyumbani.
Rais huyo wa Sudan alikuwa nchini Afrika Kusini kwa mkutano wa viongozi wa bara Afrika na kwamba serikali ilikuwa inajua kwamba ilihitajika kumkamata kwa kuwa ni mwanachama wa ICC.
Kwenye taarifa yake , ICC ilisema kuwa waranti mbili za kumkamata Bashir bado zipo.
Rais al Bashir anatafutwa na mahakama ya uhalifu wa kivita kuhusiana na uhalifu ulitokea katika jimbo la Darfur na anakabiliwa na kesi inayohusiana na uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki.
No comments:
Post a Comment