HUU ndiyo ukatili wa kutisha kufanywa na baba kwa mtoto wa kumzaa mwenyewe!
Ilikuwa vilio na simanzi kwa wakazi wa Mabibo Loyola jijini Dar kufuatia mtoto wa mwaka mmoja, William Kasuga kuchinjwa hadi kichwa kutengana na kiwiliwili kitendo kinachodaiwa kufanywa na baba yake mzazi, Maneno Kasuga, Uwazi lina mkasa wote wa kusikitisha.
WAPITA NJIA WAKWANZA KUUONA MWILI
Mwili wa mtoto William ulikutwa eneo la tukio na wapita njia ukiwa umelazwa chini ya mti huku damu zikitiririka kuashiria kwamba, tukio hilo halikufanyika muda mrefu nyuma. Ndipo wapita njia hao walipoanza kuita majirani wanaoishi eneo hilo ambao nao walikwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Kigogo-Luhanga, Dar.
WALICHOSEMA WAPITA NJIA
“Tumeshangaa sana kwa sababu tukio lenyewe ni la kusikitisha halafu mtu anakwenda kumchinja mtoto mdogo hivi! Mbona huu ni ukatili uliopitiliza kiwango jamani! Tena inaonekana huyo mtu wakati akimchinja mtoto huyu alimziba mdomo ili ashindwe kupiga kelele za maumivu wakati kisu kikipita shingoni,” alisikika mmoja wa wapita njia hao kabla haijajulikana ni mtoto wa nani na nani anatuhumiwa kuhusika.
MAMA MZAZI AFIKA ENEO LA TUKIO
Kabla polisi hawajafika, mama mzazi wa mtoto huyo, Amina Hassan (24) anayeishi Mabibo- Luhanga, Dar akiwa na baadhi ya ndugu zake waliwasili katika eneo hilo baada ya kusikia maneno kutoka kwa wapita njia kwamba kuna mtoto amechinjwa na mwili wake kutelekezwa msituni.
“Hatukuwa tukiwaza kama mtoto aliyechinjwa ni mwanangu kwa sababu tulijua alikuwa na baba yake na mara nyingi huwa anakuja kumchukua nyumbani asubuhi na kumrudisha jioni. Mimi naishi kwa mama baada ya kutokea tofauti na baba wa mtoto,” alisema mama huyo huku akimwaga machozi na kilio kikubwa.
POLISI WAWASILI
Baada ya muda, polisi walifika eneo la tukio na kumchukua mama na mwili wa mtoto huyo ambao shingo ilikuwa ikining’inia. Safari ya kuelekea Kituo cha Polisi Magomeni ilianza.
MAMA MZAZI ASIMULIA
Ilibidi Uwazi limsubiri mama wa marehemu atoke polisi na kurudi nyumbani kwake ambapo muda wa saa 12 jioni, Uwazi lilimfuata akiwa msibani tayari na kumsikia alichosema kuhusu mkasa wote.“Mimi sijui baba William aliwaza nini mpaka kuchukua uamuzi wa kumchinja mtoto wake wakati alikuwa na mapenzi ya dhati kwake.
“Pamoja na kwamba mimi nipo hapa kwa mama yangu mzazi lakini alikuwa akija na kumuomba mtoto kwenda naye kisha kumrudisha jioni.“Nakumbuka leo (Jumamosi iliyopita) asubuhi alikuja kama kawaida yake hapa akamtaka mtoto, akaondoka naye. Kutokana na mazoea hayo mimi niliona ni kawaida tu.”
ALIKUWA HANA HILI WALA LILE
“Mimi niliendelea na shughuli zangu kama kawaida hapa nyumbani. Baada ya muda nikasikia wapita njia huko nje wakisema, ‘kuna mtoto kachinjwa kwenye Msitu wa Njia ya Miti’, nikatoka mimi na ndugu zangu tukiwa na lengo la kwenda kuangalia ni mtoto gani huyo na mama yake atakuwa na hali gani!”
TAARIFA ZA KUSHTUSHA
“Lakini kabla hatujafika, tulikutana na watu njiani wakasema ni mtoto mdogo tu wa kiume, ana umri wa kama mwaka mmoja hivi. Nilishtuka sana, nikampigia simu baba yake kutaka kujua kama amesikia hilo lakini akawa hapatikani hewani.
HISTORIA FUPI
Akizungumza na Uwazi, bibi wa marehemu William, Mwanaidi Hassan alisema mwanaye alirudi kuishi kwake kutokana na kuwepo kwa ugomvi kati yake na mumewe, mtuhumiwa.“Kwa kuwa walishindwa kuelewana, mwanangu na mtoto wake wakarudi na kuishi hapa. Inaonekana mwanaume alikuwa hamwamini mkewe. Kwa hiyo mumewe akawa anakuja kumchukua mtoto na kwenda naye kisha anamrudisha jioni,” alisema mwanamke huyo.
BABA MWENYE NYUMBA
Naye baba mwenye nyumba (hakutaka kutaja jina lake) anayoishi mama wa mtoto huyo, alipozungumza na Uwazi kuhusu tukio hilo, alikuwa na haya ya kusema:“Huyu mama wa marehemu hapa ni kwa mama yake mzazi na tangu afike ana kama miezi mitatu tu lakini hatujui mume wake anapoishi kwa sababu walitokea Dodoma.
“Huyu binti alikuwa akiishi naye huko na amekuwa na kawaida ya kuja hapa karibu kila siku kwa lengo la kumchukua mwanaye na kwenda kushinda naye mchana kutwa na kumrudisha jioni.
MSIMAMO WA MAJIRANI
Watu wengi waliokuwepo msibani hapo, hasa akina mama walionekana wakisikitika juu ya kitendo hicho cha kinyama na kusema kuwa wanafanya jitihada za kupatikana kwa baba wa mtoto huyo ili wamwadabishe kwani alichokifanya ni ukatili mkubwa (hata hivyo, sheria inakataza kuchukua sheria mkononi).
“Yaani kama huyu baba atapatikana hakyamungu tutamkatakata na yeye kiungo kimoja baada ya kingine au kumbonda mawe mpaka afe. Kile ni kiumbe, maskini hakijui lolote. Leo hii mtu anakwenda kukichinja kama kuku, jamani!” alisikika mmoja wa wanawake waliokuwa wakiomboleza kifo cha kikatili cha mtoto William.
MCHEPUKO WATAJWA
Katika hatua nyingine, baadhi ya akina mama msibani hapo walidai kuwa, mara nyingi mwanaume alikuwa akimtuhumu mkewe kwamba ana mwanaume mwingine madai ambayo mke ameyakataa.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamtafuta mwanaume huyo ili kujibu madai hayo ya kumchinja mtoto wake. Marehemu William alizikwa juzi kwenye Makaburi ya Mabibo- Luhanga, Dar es Salaam. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
No comments:
Post a Comment