Tuesday, 23 June 2015

KAMATI YAKUBALI KUONDOA MUSWADA WA SHERIA YA HABARI ....

       

Muswada wa Haki ya Kupata Habari uliokuwa usomwe, kwa mara ya pili Jumamosi wiki hii, uko kwenye hatihati baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kukubali uondolewe na kurudishwa kwa wadau kwa ajili ya kuujadili kabla ya kurudishwa tena bungeni na kusomwa.
 
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alisema jana kuwa baada ya kikao na Kamati ya Bunge, wamekubaliana kuwa muswada huo uliokuwa usomwe kwa mara ya pili unatakiwa kupata baraka za wadau.

“Kamati ya Bunge ilituita, lakini tuliwaambia yetu. Muswada ni mbovu, haujashirikisha maoni ya wadau na mambo mengi hayaendani na lengo la muswada,” alisema Mukajanga.

“Tuliwaambia muswada unakuja kwa mara ya pili, lakini ni bomu, na tumeiomba Kamati ya Bunge kumwambia Spika kuwa, kwa sasa, hakuna muda wa kuujadili, tupate muda wa kuujadili zaidi, ufanyiwe kazi kikamilifu,” alisisitiza.

Hata hivyo, Mukajanga alisema kuwa Kamati itamshauri Spika kuwa kuna haja ya kuujadili pamoja na kutoa muda zaidi wa kuufanyia kazi na hakuna sababu ya kuukimbiza kupitishwa.

Kwa upande wake Deus Kibamba alisema muswada huo utabana uhuru wa upatikanaji wa habari na kwamba kuruhusu kupitishwa kwa muswada huo, kutaviweka vyombo vya habari na waandishi wa habari katika wakati mgumu kutokana na sheria na kilichomo kwenye muswada wenyewe.

Alipoulizwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kuhusu makubaliano kati ya MCT na Kamati ya Bunge ya Jamii, alisema wanasubiri taarifa kwa kuwa lazima mwenyekiti wa kamati amweleze Spika sababu za kuurudisha kwa wadau ndipo atoe uamuzi. “Kamati haina mamlaka ya kurudisha muswada kwa wadau,”alisema Dk Kashililah.

Moat waisihi Serikali 


Wakati MCT pamoja na wadau wa habari wakikutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, jijini Dar es Salaam kilifanyika kikao cha wamiliki wa vyombo vya habari ambao wameiomba Serikali kuuondoa bungeni muswada huo hadi hapo watakaposhirikishwa, kwani ukipitishwa kuwa sheria utawanyima wananchi haki ya kupata habari.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Reginald Mengi aliwaambia waandishi wa habari, baada ya kikao hicho kwamba, muswada huo ukipitishwa kuwa sheria, utavinyima uhuru wa usambazaji habari vyombo vinavyomilikiwa na watu binafsi, kitendo ambacho ni kinyume na Katiba ya nchi. “Ibara ya 5 ya Katiba inasema kila mtu ana haki ya kupata taarifa zilizopo chini ya mamlaka na kwamba kila mwenye taarifa atatoa kwa umma taarifa ambayo iko chini ya mamlaka yake,” alisema Mengi.

Alisema cha kushangaza katika ibara ya 18 ya muswada huo, kuna taarifa nyingi ambazo haziruhusiwi kutolewa zikielezwa kuwa ni kwa maslahi ya Taifa na anayekiuka na kuziandika habari hizo atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atafungwa jela miaka isiyopungua mitano.

“Huo ni mkanganyiko usioeleweka na kwa maoni yangu Serikali inajaribu kuzima uhuru wa kukusanya na kusambaza habari kwa wananchi; waandishi wengi watafungwa kama muswada huo utapitishwa kuwa sheria,” alisema Mengi.

 Kuna haraka gani kupitisha sheria inayobana uhuru wa vyombo vya habari? Tunajiuliza Serikali inataka kuficha nini?” alihoji.
 
Naye, Mfanyabiashara maarufu, Rostam Aziz anayemikiki vyombo vya habari vya New Habari (2006) Ltd, alisema muswada huo ni mbaya na utazaa sheria mbaya, hivyo ameiomba Serikali kuuondoa kwani unahitaji kuangaliwa upya na wadau ili wapate fursa ya kutoa maoni yao.

“Muswada huu utaturudisha nyuma kama taifa, hivyo hakuna haja ya kujadili kifungu kimoja kimoja kwani vingi vina athari kwa wadau wa wahabari na wananchi. Tunaomba Serikali iuondoe bungeni muswada huu,”alisihi.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication Ltd (MCL), Francis Nanai na Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.

Akitoa ufafanuzi wa muswada huo, Mwanasheria kutoka Kampuni ya Maleta and Ndumbalo Advocate, Dk Damas Ndumbalo alisema katika muswada huo kuna mambo mengi yanatajwa kama yenye maslahi kwa Taifa ambayo hayatatakiwa kutolewa kama taarifa.

Miongoni mwa taarifa ambazo zina maslahi kwa Taifa ambazo hazitakiwi kuripotiwa ni yoyote itakayoathiri uendeshaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC). Kwa mujibu wa Dk Ndumbalo, muswada huo ukiwa sheria, utakuwa kikwazo kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao.

Akifafanua zaidi, Dk Ndumbalo alisema kifungu cha 11 na 12 cha muswada huo kinatoa muda wa siku 30 mamlaka husika kukupa taarifa ulizoomba. “Siku zote thelathini unasubiri taarifa uliyoomba, sasa hiyo itakuwa bado habari?”alihoji.

No comments:

Post a Comment