WAZIRI WA FEDHA WA TANZANIA SAADA MKUYA SALUM ..
Bajeti ya Serikali ya 2015/16 inayoanza kujadiliwa bungeni leo huenda isitekelezeke kama inavyotarajiwa kutokana na changamoto za kisiasa zitakazoathiri ukusanyaji wa mapato.
Wataalamu wa masuala ya uchumi wamesema hayo
katika hafla ya uchambuzi wa bajeti iliyoandaliwa na Kampuni ya Ukaguzi
wa Hesabu ya KPMG na kuongeza kuwa Uchaguzi Mkuu na maandalizi hafifu ya
baadhi ya vyanzo vya mapato yatasababisha Serikali kutotimiza malengo
yake.
Profesa wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe,
Honest Ngowi alisema Uchaguzi Mkuu, hatima ya Kura ya Maoni, mbio za
urais na matarajio ya Oktoba yatazorotesha kwa kiasi kikubwa utekelezaji
wa bajeti hiyo.
“Hii ni bajeti ya sherehe ya kuagwa (send off)
lakini pia ya fungate. Kwa kipindi hiki tulichopo wanasiasa hawatakubali
wananchi wanyanyasike kulipa ushuru na kodi lukuki wakati ndiyo
wapigakura wao.
“Tusitarajie kuona nidhamu ya utekelezaji wa
bajeti kama tulivyozoea kwa sababu ya kubadilika kwa utawala,” alisema
Profesa Ngowi.
Alisema katika kipindi hicho kutakuwa na ulegevu
katika utumishi wa umma na taasisi zinazotakiwa kuikopesha Serikali
zitakuwa zikisubiri kuona mabadiliko ya uongozi ili kujihakikishia
usalama wa malipo yao.
Kuhusu mpango wa Serikali kutumia risiti za
kielektroniki kuongeza mapato ya idara na Serikali za Mitaa, Profesa
Ngowi alisema kuna wasiwasi wa taasisi kutokuwa na mashine za kutosha
kufanikisha hilo.
“Kama hujajenga uwezo wa kufikia malengo ya
kukusanya fedha hizo kwa nini unatishia kuwaadhibu?” alihoji huku
akibainisha kuwa agizo la Serikali Kuu kwa Serikali za Mitaa kutotoa
zabuni kwa kampuni zisizotumia EFD si la busara kwa kuwa mashine hizo
bado zina mgogoro ambao haujapatiwa suluhu.
Meneja wa Kodi wa KPMG, Nsanyiwa Donald alisema
hakuna mabadiliko makubwa katika mfumo wa kodi ikilinganishwa na mwaka
2014/15 zaidi ya kuongeza kodi katika mafuta ya petroli na kuanza
kutumika kwa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) Julai.
Alipoulizwa iwapo kulikuwa na vyanzo vingine vya
mapato badala ya kuongeza kodi katika mafuta, Donald alisema Serikali
ilikuwa na uwezo wa kuachana na kodi hiyo na kuanzisha tozo kwa wamiliki
wa nyumba.
Bajeti hiyo ya Sh22.4 trilioni ambayo inaanza
kujadiliwa leo, inaweza kupata changamoto za wabunge kutokana na
kutopatikana kwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya kukamilisha au
kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kabla ya kuanza uchambuzi huo, Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia atawasilisha Bajeti ya Kambi ya Upinzani.
No comments:
Post a Comment