Wednesday, 24 June 2015

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA BURUNDI AHOFIA USALAMA ...

  Makamu wa pili wa rais wa Burundi, Gervais Rufyikiri, ambaye ametangaza kujiuzulu kwenye wadhifa wake.

Makamu wa pili wa rais nchini Burundi, Gervais Ruyikiri ametangaza kuwa hatorurudi nchini kama usalama wake utakua haujalindwa ipasavyo. 

Akizungumza kwenye televisheni ya Ufaransa France 24, Gervais Rufyikiri, amesema ameamua kufanya hivyo akihofia usalama wake kutokana na jinsi hali invyoendelea nchini Burundi.

Gervais Rufyikiri, ambaye ni mmoja wa vigogo wa chama tawala cha Cndd-Fdd amesema amemuandikia barua rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, akimuomba kuachana na mpango wake wa kuwania muhula wa tatu, akibaini kwamba ni kinyume na Katiba ya nchi pamoja na Mkataba wa amani na maridhiano wa Arusha.

Gervais Rufyikiri amesema rais Nkurunziza amekua hasikii hata nasaha anazopewa na taasisi za kimataifa pamoja na washirika wake wa karibu.
Wakati huo huo Spika wa Bunge la Burundi, Pie Ntavyohanyuma ameondoka nchini humo Jumatano Juni 24, akielekea nchini Ubelgiji. 

Haijafahamika iwapo kiongozi huyo wa taasisi muhimu nchini ameitoroka nchi hiyo au la. Lakini habari ambazo zimeendelea kusambaa mjini Bujumbura zinabaini kwamba Pie Ntavyohanyuma ameitoroka nchi.

Hayo yakijiri serikali ya Bujumbura ikiwakilishwa na waziri wake wa mambo ya ndani, Edouard Nduwimana, imeshiriki katika mazungumzo yanayolenga kutafutia ufumbuzi mgogoro unaoendelea kushuhudiwa nchini Burundi.

Mazungumzo hayo yameingia Jumatano wiki hii katika siku yake ya pili, baada ya kuanza Jumaanne Juni 23.

Katika siku yake ya kwanza, mazungumzo hayo yaliitikiwa na upinzani, mashirika ya kiraia pamoja na viongozi na wawakilishi wa dini mbalimbali.
Serikali ya Bujumbura na chama tawala pamoja na baadhi ya washirika wake walisusia mazungumzo hayo, wakibaini kwamba hawatashiriki mazungumzo hayo ambayo yanakuja kuwapotezea muda wakati ambapo wako katika siku za mwisho za kampenzi za uchaguzi wa wabunge na madiwani.

Jumatatu wiki hii timu ya usuluhishi iliwatolea wito wadau wote katika mgogoro wa Burundi kushiriki mazungumzo kwa minajili ya kutafutia suluhu mgogoro huo. Lakini Chama tawala cha Cndd-Fdd na serikali vimesusia kikao cha kwanza cha mazungumzo hayo.

Jumanne Juni 23 chama hicho cha rais Pierre Nkurunziza kilitangaza kuwa hakitashiriki kutokana na kampeni ya uchaguzi wa wabunge na madiwani ambayo kinaendesha wakati huu zikisalia siku zisiozidi sita ili ufanyike uchaguzi wa wabunge na madiwani.

Chama cha Uprona kinachotambuliwa na utawala wa Pierre Nkurunziza hakikushiriki mazungumzo hayo.

Kwa mujibu wa katibu mkuu wa chama cha Uprona, Gaston Sindimwo, huu siwakati wa mazungumzo. " Mazungumzo yanakaribishwa baada ya uchaguzi, hapana wakati huu", amesema gaston Sindimwo.

Itafahamika kwamba chama cha Cndd-Fdd kimekua kikifutilia mbali uwezekano wowote wa kuandaa kwa makubaliano ya wadau wote katika mchakato wa uchaguzi kalenda ya uchaguzi, pamoja na kuanzisha mazungumzo yatakayowashirikisha wadau wote.

Timu ya usulihishi wa kimataifa ilikutana Jumatatu wiki hii kwa mara ya kwanza mjini Bujumbura. Timu hii inaundwa na Ibrahima Fall kutoka Umoja wa Afrika, Abdoulaye Bathily kutoka Umoja wa Mataifa, Katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Richard Sezibera pamoja na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR ).

Hayo yakijiri hali ya usalama imeendelea kudorora katika maeneo mbalimbali nchini Burundi, hususan katika mji mkuu wa Bujumbura.
Hali ya hofu imeendelea kutanda katika mji wa Bujumbura, huku kila upande ukiutuhumu mwengine kuhusika na mdororo wa usalama unaoshuhudiwa wakati huu nchini Burundi.

No comments:

Post a Comment