Sunday, 14 June 2015

ASKARI 13 WA AL SHA BAAB WAUWAWAA KENYA ....

Wapiganaji 13 wa Alshabaab wameuawa baada yao kushambulia kituo cha kijeshi cha Baure kilichoko eneo la Lamu katika pwani ya Kenya.
Msemaji wa jeshi la Kenya kanali David Obonyo ameithibitishia BBC kuwa wapiganaji hao walivamia kambi hiyo ya kijeshi mwendo wa 5:45 alfajiri ya leo lakini wakazidiwa nguvu kabla hawajaingia ndani ya kambi hiyo.

Kanali Obonyo alisema kuwa wawili kati ya wale waliouawa ni wenye asili ya kizungu.
Hakuna aliyepatikana hai japo washambuliaji wengine wa Al Shabaab wanasemekana kutorokea katika msitu mkubwa wa Bony ambapo wanajeshi wanawafwata.

                       
Shambulizi hili linawadia siku ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kutokea shambulizi la Mpeketoni Lamu
Kanali Obonyo amesema kuwa wamepata zana kali na za kisasa za kivita.
Aidha amethibitisha kuwa wanajeshi wawili wa Kenya waliokuwa wakishika doria waliuawa katika shambulizi hilo.

Shambulizi hilo limetokea huku wakenya wakiadhimisha mwaka mmoja tangu wapiganaji wa Al shabaab waliposhambulia mji wa mpeketoni na kuua zaidi ya watu sitini katika eneo hilohilo la Lamu.

Hapo jana, Serikali ya Kenya ilitangaza kuanzisha operesheni kukabili tishio la kigaidi wakati wa mfungo wa kiislamu wa Ramadhan.

Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Kenya, Joseph Boinet alisesema japo sio wajibu wa Kenya kushika doria na kulinda usalama ndani ya kambi za wakimbizi zilizoko nchini Kenya,

''imewalazimu kuchukua hatua kali kudhibiti utovu wa usalama kufuatia habari za kijasusi zilizodai kuwa wanamgambo wa Al Shabaab wanatumia kambi hiyo ya wakimbizi kubwa zaidi nchini Kenya kupanga mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya''. Alisema Boinet.


                       
Inspekta Jenerali wa Polisi alitangaza hali ya tahadhari baada ya kupokea habari Al shabaab wanapanga shambulizi wakati wa Ramadhan
Boinet alisema hali ya usalama imeimarishwa vilivyo kufuatia vyanzo vinayoaminika kudai kuwa kundi hilo la Jihad linapanga kutekeleza mashambulizi wakati wa mfungo wa dini ya kiislamu wa Ramadhan.

''Wanataka kuvuruga amani wakati wa kipindi hiki cha dua takakatifu kwa wakenya wasio na hatia kwa kutekeleza mashambulizi na mauaji, lakini tumechukua tayadhari kubwa.''

''Tumeimarisha usalama katika taasisi za umma ,vyombo vya usalama, taasisi za mafunzo, makanisa, masoko na maduka makubwa hasa mjini Nairobi, Mombasa and Kaskazini kwa Kenya''
'' Inaumiza sana kuwa wakimbizi ambao tumewapokea katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya wamegeuka na kuanza kushiriki uhalifu na hata kuumiza wenyeji wao.''

Inspekta huyo mkuu alisema kuwa tahadhari hiyo inafuatia vyanzo kamilifu vya kijasusi.
''Sio wajibu wetu kulinda usalama ndani ya kambi lakini sasa imetubidi kuwa waangalifu zaidi kujua nani anaingia ndani ya kambi hizo na ni nani anayetoka humo'' aliongeza Boinnet.

Amesema kuwa serikali ya Kenya imeimarisha uwezo wake wa kupambana na shambulizi lolote la kigaidi ikiwemo kudukua mawasiliano yao kupitia njia ya mitandao ya kijamii ya Facebook na WhatsApp.

Serikali ya Kenya imekuwa ikilaumu kuwepo kwa wakimbizi wengi wenye asili ya Somalia ndani ya mipaka yake kwa utovu wa usalama.

No comments:

Post a Comment