Friday, 26 June 2015

ENYEMA na KOCHA WAWEKWA KITI MOTO ....!


Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) limewaweka kitimoto kipa wao mkongwe, Vincent Enyeama na kocha Stephen Keshi kwa madai ya utovu wa nidhamu na kukiuka kanuni za maadili walizosaini.

Enyeama, 32, anayeongoza kwa kuchezea zaidi timu ya taifa – Super Eagles, anashitakiwa kwa kusema hadharani kwamba hawakutakiwa kucheza jijini Kaduna dhidi ya Chad, akieleza kwamba usalama haungekuwapo.

Hiyo ilikuwa wakati wa mechi ya kwanza ya kutafuta kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017. Keshi anatakiwa kujibu mashitaka ya kuomba kazi ya kuifundisha Timu ya Taifa ya Ivory Coast, muda mfupi tu baada ya kupewa kazi ya kudumu na NFF.

Enyeama anasema kwamba alidhani suala lake limemalizika kwa sababu alitakiwa aombe radhi na kufanya hivyo mara moja, lakini sasa NFF inahoji kwa nini hakufika kwenye kikao cha kusikiliza kesi yake wiki hii.

Kipa huyo anasema kwamba wala hajapata barua inayomwita kwenye kikao hicho. Keshi kwa upande wake anadai kwamba hajapata kuomba kazi Ivory Coast, bali wakala ambaye hata hivyo hakumtaja jina, ndiye alipeleka maombi hayo bila kumuarifu.

Ivory Coast wanatafuta kocha kwa ajili ya timu yao ya taifa – Tembo – na baada ya makocha au mawakala kutuma maombi, shirikisho la soka la huko lilibandika hadharani majina ya makocha 59 walioomba, wakiwamo Wafaransa na Waitaliano wengi, Mwingereza mmoja na Keshi.
Ivory Coast wanatafuta mrithi wa Herve Renard aliyewapa ubingwa wa Afrika na kisha kuondoka kwa ajili ya kufanya kazi nchini Ufaransa.

Ofisa wa ngazi za juu wa NFF, Chris Green amenukuliwa na vyombo vya habari vya Nigeria akisema kwamba watatuma ujumbe Abidjan, Ivory Coast kwa ajili ya kupata ukweli juu ya uombaji kazi wa Keshi kabla ya shauri lake kusikilizwa.

Kamati ya Utendaji ya NFF itatoa uamuzi baadaye juu ya mchezaji na kocha huyo, lakini bado haijasema ni lini itafanya hivyo. Mechi nyingine ya kufuzu kwa AFCON baina ya Nigeria na Misri imepangwa pia kufanyika jijini Kaduna.

Nigeria imekuwa ikiandamwa na mashambulizi ya kigaidi kutoka kwa genge la Boko Haram katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, na ni kwa sababu hiyo Enyeama alitaka mechi ifanyike eneo lenye usalama zaidi.

No comments:

Post a Comment