Wema alisema kwa muda mrefu marehemu baba yake
Balozi Issac Sepetu, alikuwa akimshauri aingie kwenye siasa na sasa
ametimiza ndoto za wazazi wake.
Miaka mitano iliyopita, Wema anayekubalika na
mashabiki wengi, aliwahi kuweka wazi kuwa yeye ni mkereketwa wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) na mshabiki wa klabu ya soka ya Yanga na kwamba hiyo
ndiyo sababu ya yeye kupendelea rangi za njano na kijani.
Akizungumza na kipindi cha redio cha Ala za Roho
kwa njia ya simu, usiku wa kuamkia jana, Wema alisema yupo mkoani
Singida kwa muda sasa akiendelea na kampeni ili kujitayarisha kuchukua
fomu ifikapo Julai 15 mwaka huu.
Alisema anaamini nguvu za Mungu, Watanzania na
watu wa Singida watamwamini na kumpa kura zao kwa kuwa sasa ni wakati wa
vijana kujipambanua na kusaidia jamii yao.
“Nipo Singida kuhamasisha vijana wajitokeze
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Kupiga Kura, pia huku mimi ni
nyumbani na nimejiandikisha tayari, ili ifikapo Julai 15 nichukue fomu.
Ninachotafuta ni kuungwa mkono na Watanzania,” alisema Wema.
Alibainisha kuwa anajiamini na hakuna
kitakachomshinda, kwani alipoingia katika mashindano ya ‘Miss Tanzania
hakutegemea kama ataweza, lakini alifanikiwa, hata alipojitosa kwenye
uigizaji akafanikiwa.
“Sasa naingia katika siasa, najua kwamba nitaweza.
Mimi ni binadamu, nina mambo yangu, ila naamini hakuna
linaloshindikana. Nitagombea ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida,
Inshallah tuombe uzima,” alisema.
Wema alisema kwamba tayari ana kikundi chake cha kampeni akiwamo meneja wake Martin Kadinda sanjari na Petitman Wakuache.
“Nimeshafanya mengi kuhusu kujiandaa na uchaguzi
hata kampeni, nilikuwa nazungumza na uongozi wangu ambao yupo Martin
Kadinda pia yumo Petiman, huyu anahusika na kampeni yangu kwa hiyo
Watanzania wajue tu kwamba nitachukua fomu ya kugombea ubunge wa Viti
Maalumu na tutaona huko mbele itakavyokuwa kwa sababu hiki ni
kinyang’anyiro,” alisema Wema.
Wema alisema kwamba kwa sasa ni kama anaingia kwenye mapambano yaliyo sawa na vita hivyo kuna kupata na kukosa.
“Lakini sifikirii kukosa kwa sababu mtu ukifikiri
kukosa unajiweka kwenye ‘negative side’, lakini najua kwa nguvu za
Watanzania na kwa nguvu za wananchi wa Singida, wataniamini na kunipa
kura zao,”alisema.
Wema alifafanua kwamba licha ya kuungwa mkono na wanaume wengi
mkoani humo, kinamama wa Singida pia wanamuunga mkono kwani wanamfahamu
vizuri na sera zake wanazijua, hivyo ahofii kelele za watu wa pembeni.
“Nitaingia bungeni kwa ajili ya maslahi ya
wananchi na kutetea haki za wananchi wangu, si kingine. Wamejitokeza
watu wengi kwa ajili ya kugombea, kwa nini amejitokeza Wema Sepetu na
watu wameanza kuzungumza mambo mengi?” alihoji.
Katika mahojiano hayo Diva alimuuliza Wema Sepetu kuhusu taarifa ya kuwa na uhusiano na rafiki wa kiume wa Linah alisema:
“Huwezi kuamini, habari hizo siyo za kweli kwa
sababu tulikuwa tunafanyakazi naye tu, ila nimeshangazwa kuona kwa nini
Linah ameenda hewani kwenye kipindi na kuzungumza hizo habari, naomba
watu waelewe kwamba si kweli.”
No comments:
Post a Comment