Tuesday, 16 June 2015

KEJELI YA WAPINZANI KUHUSU BAJETI YA TAIFA ...

Kambi rasmi ya upinzani bungeni imesema Serikali inatakiwa kukusanya Sh19.6 trilioni kwa mwaka tofauti na malengo iliyojiwekea ya Sh13.4 trilioni, huku ikihoji sababu za miradi ya maendeleo kutegemea mikopo ambayo alisema imeongeza ukubwa wa deni kwa wananchi.
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti Mbadala jana, Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia alisema lengo hilo linaweza kufikiwa endepo Serikali itaweka mazingira mazuri na rafiki kwa mlipakodi.

Mbatia, aliyeingia kwa staili ya aina yake akionyesha mkoba uliobeba bajeti, alisindikizwa na Mchungaji Peter Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini, Moses Machali (Kigoma Kasulu), Salum Barwani (Lindi Mjini) na Mustapha Akonay (Mbulu).

Mbatia alitaja njia nyingine za kuongeza mapato kuwa ni kupunguza misamaha ya kodi isiyokuwa na tija hadi kufikia asilimia moja ya Pato la Taifa, kuongeza ufanisi Bandari ya Dar es Salaam na kuweka mazingira mazuri na endelevu katika sekta ya utalii.

Mbatia alirejea wito wa kila mwaka wa wapinzani wa kutaka juhudi zaidi kuwekwa katika kupanua wigo wa vyanzo vya mapato katika sekta kama uvuvi, maliasili, nyumba na ardhi.

Alisema Serikali ipanue wigo wa kodi, kuweka sera na viwango vya kodi vinavyotabirika na endelevu, kuongeza ufanisi wa TRA kwa asilimia 50 na kudhibiti ukwepaji wa kodi.

“Tutaweza kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi hadi kufikia asilimia 20 mpaka 25. Washindani wetu wakubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki wanakusanya mapato kwa asilimia 22 ya Pato la Taifa, na hawana mazingira mazuri ya uwekezaji na rasilimali nyingi kama Tanzania,” alisema Mbatia.

Mbatia aliendelea kubainisha sura ya bajeti mbadala kuwa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yatakuwa ni Sh18 trilioni na mapato ya halmashauri kuwa Sh848.1 bilioni. Alisema mikopo na misaada ya kibajeti ni Sh660 bilioni huku mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo ikiwa ni Sh1.6 trilioni.

Msemaji huyo wa Kambi ya Upinzani alilinganisha bajeti ya Serikali na bajeti mbadala na kusema bajeti mbadala haina mikopo ya kibiashara, hivyo inalenga kulipunguzia taifa mzigo wa madeni.

“Bajeti ya Serikali ina mikopo ya kibiashara ya asilimia 10, bajeti hii inawaongezea wananchi mzigo wa madeni,” alisema Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.

Alisema hivi sasa kila Mtanzania anadaiwa Sh873,904.56 kutokana na deni la Taifa kuzidi kukua.

Kuhusu kutotekelezwa kwa miradi ya maendeleo, Mbatia alisema hali hiyo ilitokana na wahisani kusitisha misaada na hiyo ni kutokana na kashfa mbalimbali.
“Kutokana na kashfa ya ufisadi wa miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow, wahisani walisitisha misaada ya bajeti kwa hoja kuwa viongozi wa Serikali walipanga na kufanikisha mbinu za kuliibia Shirika la Umeme (Tanesco) lenye matatizo makubwa ya kifedha,” alisema.

“Hadi kufikia Aprili 2015, wahisani waliipa serikali mikopo na misaada ya kibajeti ya Sh406 bilioni ukilinganisha na ahadi ya Sh922 bilioni, sawa na asilimia 40. Serikali imepokea mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo Sh 1.4trilion ukilinganisha na bajeti ya Sh2.0 trilioni sawa na asilimia 70 ya bajeti.

“Mikopo yenye masharti ya kibiashara haikupatikana kama serikali ilivyotarajiwa, lakini swali la kujiuliza, kwenye nchi yenye rasilimali za kutosha inawezaje kuweka mikopo kama mojawapo ya vipaumbele cha vyanzo vya uendeshaji wa bajeti yake? Hili ni jambo la aibu kubwa, kuona kuwa Serikali inashindwa kutekeleza miradi yake ya maendeleo kwa kuwa walipoomba kukopa, mikopo hiyo haikutolewa.”

Alisema miradi ya maendeleo ndiyo iliyoathirika zaidi kwa kuwa hadi kufikia Aprili 2015 ilikuwa imepata asilimia 40 tu ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge wakati matumizi ya kawaida yalikuwa asilimia 86.

“Swali la kujiuliza, unaendeshaje uchumi ambao hauna fedha za miradi ya maendeleo lakini fedha za mishahara na posho zinaendelea kulipwa?” alihoji.

Serikali imepanga kupunguza utegemezi wa fedha za wahisani hadi kufikia asilimia 6.4 ya bajeti ya mwaka 2015/16, wakati inatarajia kupata misaada na mikopo nafuu ya Sh2,322.5 bilioni kwa mwaka huu wa fedha, kiwango ambacho ni asilimia 10 ya bajeti.

Ukokotoaji bajeti

Akiwasilisha bajeti hiyo huku akipigia chapuo Ukawa kuchukua nchi, Mbatia alisema kutokana na takwimu za Benki Kuu za Juni 2014 na Juni 2015, thamani ya shilingi moja ya Juni mwaka  jana  inazidi Sh1.2 ya leo. Kwa hiyo Sh19.85 trilioni za Juni 2014  thamani yake kwa sasa ni zaidi ya Sh24 trilioni za leo.

Alisema tofauti kati ya mwaka 2014/2015 na 2015/2016 ni Dola 1,143.89 milioni za Kimarekani, sawa na Sh2.36 trilioni. “Punguzo hili ni sawa na asilimia 9.5. Hivyo, leo Serikali inapojigamba kuwa bajeti imeongezeka kutoka Shilingi 19.85 trilioni kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 kufikia Sh22.5 trilioni kwa mwaka wa fedha 2015/2016 siyo sahihi. 

“Kwani inasahau kuwa thamani ya shilingi ya leo ni pungufu ya thamani ya shilingi ya mwaka jana. Hii ina maana kuwa bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2015/2016 ni ndogo kuliko bajeti ya mwaka 2014/2015… Kambi ya Upinzani inasikitishwa na kitendo cha Serikali kushindwa kuwaeleza Watanzania ukweli wa ongezeko hasi la bajeti ambalo haliendani na thamani ya Shilingi kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016,” alisema.

“Kitendo cha Serikali hii kuwadanganya Watanzania kwa kuwapa tumani hewa ya ongezeko la bajeti ni cha kupingwa kwa nguvu zote na watu wote kwa manufaa ya Mama Tanzania.”

Mbatia alisema Serikali hukusanya mapato kutoka kwa walipa kodi, kwa uadilifu na kupanga  kutumia mapato hayo, kwa uangalifu; katika maeneo yatakayostawisha jamii nzima na kusema kinyume na matarajio ya wengi, Serikali  imeshindwa kutimiza malengo yake,  ikiwemo kukusanya kodi bila uadilifu na hivyo kuchochea vitendo vya rushwa, ufisadi na ubadhirifu.
“Serikali hii imeshindwa kutimiza ahadi yake ya maisha bora kwa kila Mtanzania na badala yake jamii ya Kitanzania sasa inashuhudia ongezeko la kasi la mfumuko wa bei, ukosefu wa fedha za kigeni na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yake. Kuyumba huku kwa uchumi, kumewaumiza Watanzania wa makundi yote,” alisema.

“Matatizo yaliyopo ni ukosefu wa nidhamu na uwazi katika masuala ya bajeti. Kipindi hiki Taifa linashuhudia uwepo wa ongezeko la malimbikizo ya malipo; bajeti inayopitishwa na Bunge haifanani na bajeti inayotekelezwa na Serikali; makadirio ya mapato ni makubwa kuliko ukusanyaji wa mapato halisi na ongezeko holela la misamaha ya kodi.

“Pia bajeti ni tegemezi na matumizi ya kawaida ni makubwa kuliko mapato ya Serikali; matumizi ya kawaida ni zaidi ya fedha za miradi ya maendeleo; kuongezeka kwa kasi ya ukuaji  wa deni la taifa; ongezeko la vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma yanaainishwa na CAG, lakini hakuna hatua za kisheria na za  kinidhamu stahiki zinazochukuliwa.”

No comments:

Post a Comment