Wednesday, 18 February 2015

AZAM YANGA KATIKA MTIHANI MWINGINE ..> source MTANZANIA


 http://mtanzania.co.tz/wp-content/uploads/2015/02/Yanga-Vs-Azam.jpg 
AZAM FC
http://mtanzania.co.tz/wp-content/uploads/2015/02/yang.jpg
 DAR YOUNG ..

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom, Azam FC na Yanga leo wanatarajia kuendeleza vita ya ubingwa kwenye ligi hiyo.

Yanga watakuwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kuvaana na Tanzania Prisons ya huko, huku Azam ikipepetana na Ruvu Shooting katika Uwanja wa Mabatini, Pwani.

Kitu kinachonogesha mechi hizo ni vita ya ubingwa iliyopo baina ya Yanga na Azam, ambazo zote zinakabana koo kileleni zikiwa na pointi 25.

Lakini Azam ipo kileleni kutokana na uwiano mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Timu hizo zitaingia dimbani zikiwa na kumbukumbu ya kufanya vizuri kwenye michezo yao ya michuano ya Afrika iliyofanyika wikiendi iliyopita, ambapo Azam iliichapa El Merreikh ya Sudan mabao 2-0 katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga yenyewe ilipata ushindi kama huo wa Azam kwa kuifunga BDF XI ya Botswana kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Vile vile kwenye michezo iliyopita ya ligi, timu hizo zilicheza na Mtibwa Sugar, ambapo Yanga ilianza kwa kuwachapa mabao 2-0, huku Azam ikiipa kisago cha mabao 5-2.

Akizungumza na MTANZANIA, Kocha Msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema mechi yao dhidi na Prisons itakuwa ngumu, hivyo akawataka mashabiki wa timu hiyo kutanguliza maombi.

“Timu nyingi zimeonyesha kujipanga vizuri katika mzunguko huu wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom, hivyo wao kama makocha wamewaelekeza wachezaji wao wanachotakiwa kukifanya uwanjani.”
“Hii mechi ni ngumu, pia ikumbukwe kwamba, Prisons wapo nyumbani na wanahitaji pointi tatu na sisi tunahitaji pointi tatu ili zitufikishe kileleni, hivyo mechi hii ni ngumu na tunachohitaji ni maombi tu,” alisema.
Prisons ikipoteza mchezo wa leo basi itazidi kujichimbia kaburi, kwani mpaka hivi sasa ipo mkiani mwa msimamo ikiwa na pointi 11.

Ili kuwatia moyo mashabiki wa soka Mkoa wa Mbeya, Katibu Mkuu wa Prisons, Oswald Morris, aliwataka kutokata tamaa na kikosi hicho kwani mpira ni dakika 90, ambazo wanaamini zitazaa matunda.

“Kikosi kimejipanga vizuri lakini nguvu kubwa inategemewa kutoka kwa mashibiki, hivyo tunawaomba wajitokeze kwa wingi uwanjani kuwashangilia wachezaji,” alisema.

Naye Kocha Mkuu wa Azam, Joseph Omog, alisema mechi yake dhidi ya Ruvu Shooting itakuwa ngumu, lakini amejinasibu kuzoa pointi zote tatu na kuendeleza matumaini yao ya kutwaa ubingwa.


“Huu ni mzunguko wa pili wa ligi, unapopoteza mchezo unaipa nafasi timu iliyopo chini yako kukuzidi, hivyo natarajia kufanya vizuri tena kesho (leo) dhidi ya Ruvu Shooting,” alisema.

Azam itaingia dimbani ikiwa bila beki wake kisiki, Aggrey Morris, ambaye leo atamalizia adhabu yake ya kutocheza mechi tatu za ligi akidaiwa kumpiga kiwiko kwa makusudi, Emmanuel Okwi (Simba) na kumfanya kukimbizwa hospitali baada ya kuzimia kwa takribani dakika tano.

Matokeo yoyote mabaya kwa Azam au Yanga leo yatafanya mmojawapo kuzidiwa pointi na mwenzake, huku pia akitoa nafasi ya kusogelewa na timu za chini ambazo ni Kagera Sugar (pointi 21) na Simba (pointi 20) kama zitashinda mechi zao za wikiendi hii.

No comments:

Post a Comment