Morogoro. Mauaji yanayotokana na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro, yanazidi kutikisa baada ya watu wengine watatu kuuawa kwenye Kijiji cha Mbiligi, Kata ya Magole wilayani Kilosa.
Tukio hilo, ambalo limetokea mwezi mmoja tu baada
ya mkulima mmoja kuuawa kwenye Bonde la Mgongola wilayani humo, ni kati
ya matukio mengi ya mapigano baina ya jamii hizo mbili na ambayo
yalijadiliwa kwa kina kwenye mkutano uliopita wa Bunge la Muungano.
Habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa, juzi
saa 2.00 asubuhi wakulima wapatao 15 walikwenda eneo la Matembele na
Ming’oni, jirani na Kijiji cha Mbigili ili kupanda mpunga, lakini saa
nne baadaye vijana wawili wa Kimasai walifika na kuhoji sababu za
kutumia eneo hilo kwa kilimo wakati ni mali ya Kijiji cha Mabwegela na
kuwaamuru waondoke.
Lakini wakulima hao walikaidi na ndipo muda mfupi baadaye likaibuka kundi la wafugaji wapatao 50 na kurejea swali hilo.
Habari hizo zilisema kuwa, baada ya wakulima kuona
wamevamiwa, walianza kuwarushia Wamasai mapande ya udongo na
walipozidiwa ndipo waliporudi nyuma, lakini ghafla wakajikuta
wamezingirwa.
Kwa mujibu wa habari hizo, wakulima waliamua
kutoroka, ndipo baadhi yao waliposhambuliwa kwa mikuki, virungu, mishale
na visu na kusababisha vifo vya watu hao watatu.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo alisema
watu wengine kadhaa walijeruhiwa na wamelazwa katika Kituo cha Afya cha
St Joseph cha Dumila, Kilosa.
Alisema waliouawa ni Joseph Lawama, ambaye ni
mkulima wa Mbigili (26), Rajabu Kigongo, mkulima wa Mbigili ambaye
alichomwa mshale mgongoni na kuchanwa na shingoni na Kandura Kashu (30)
mfugaji wa Mabwegere.
Alisema mtu mmoja alifariki dunia katika maeneo ya
tukio na wengine wawili wakati wakitibiwa katika kituo cha afya. Pia
aliwataja majeruhi kuwa ni Binzi Dotto (42), Juma Someke (35) na Mohamed
Selemani (36).
“Mgogoro huu unatunyima usingizi viongozi katika
jitihada zetu za kuutatua na kuepusha umwagaji damu. Tumekuwa
tukijitahidi kuitisha vikao vya upatanishi kati ya vijiji vya Mbiligili
na Mabwegere, lakini hakujawa na mafanikio,” alisema Tarimo.
Alisema tatizo hilo linatokana na baadhi ya viongozi wa Kijiji cha Mabwegere kukataa kuhudhuria vikao vya upatanishi.
Muuguzi wa zamu katika Kituo cha Afya cha St
Joseph, Melania Shayo alisema walianza kuwapokea majeruhi saa 10.30
jioni na kwamba wakati wakiwahudumia, wawili walifariki dunia.
No comments:
Post a Comment