Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani Mara ilisema askari huyo MT-78227, aliokotwa katika eneo la jeshi Januari 30, mwaka huu saa sita mchana mwili wake ukiwa hauna baadhi ya viungo ukiweamo mguu wa kulia, viganja vya mikono yote na sehemu za siri.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ernest Kimola, alisema upande wa mguu wa kushoto wa marehemu ulikutwa na jeraha lililokatwa na kitu chenye ncha kali hali inayoonyesha huenda askari huyo aliuawa na kutupwa kwenye eneo hilo.
Alisema huenda viungo vya askari huyo ambavyo havikukutwa vilikuwa vimeliwa na wanyama baada ya mwili huo kuonekana kukaa muda mrefu, kuanza kuharibika na kuingiliwa na wadudu.
“Baada ya kupata taarifa za tukio hilo polisi walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa askari huyo kwa ajili ya taratibu nyingine zitakazofanyika.
“Natoa wito kwa wananchi watakaokuwa na taarifa juu ya tukio hili kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ili kuweza kubaini chanzo na taarifa zaidi na wahusika wa tukio waweze wakipatikana wafikishwe kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi,” alisema Kimola.
Kamanda wa Kikosi cha 27 KJ Makoko ambaye alikataa kutaja jina lake kwa madai kuwa si msemaji, alisema tukio hilo ni la kusikitisha na akasema askari yeyote achukuliwe kama mlinzi wa amani na si jambo jema kufanyiwa unyama kama huo.
Alisema huenda askari huyo aliuawa na kutupwa kwenye eneo la jeshi pembeni ambako si rahisi watu kuwaona waliofanya tukio hilo.
“Nawaomba askari wasipende kutembelea maeneo hatarishi hususan nyakati za usiku kwa kuwa wako watu ambao si wazuri ambao huweza kufanya jambo lolote kwa askari bila kutambua umuhimu wake katika kutekeleza majukumu yake ya uaskari.
“Hilo la kukutwa sehemu ya viungo vya mwili vikiwa havipo huenda ni imani za ushirikina kwa kuwa wanadamu wa leo wamebadilika na kufanya vitu visivyofaa lakini naamini suala hili litafuatiliwa na vyombo vinavyohusika kujua undani wake,” alisema.
No comments:
Post a Comment