Mwanamuziki nyota wa kike nchini, Lady Jaydee jana aliamua kuwaburudisha mashabiki wake kwa staili ya kipekee; kuzungumzia kuvunjika kwa ndoa yake na Gadner Habash.
Kwa muda mrefu kumekuwa na minong’ono kuwa wawili hao wametengana, lakini hakuna aliyekuwa tayari kuweka wazi kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, jana, Jaydee, ambaye jina lake halisi
ni Judith Wambura aliamua kutoa ya moyoni, akisema kuwa kwa sasa
ametengana rasmi na mtangazaji wa kituo cha redio cha E-fm cha jijini
Dar es Salaam.
Jaydee ambaye wakati mwingine huitwa ‘Jide’, kwa
wiki moja sasa ameamua kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa mashabiki
wake kwenye mitandao ya kijamii.
Kati ya maswali aliyoulizwa na mashabiki wake ni kama ni kweli ametengana na mumewe na ni sababu za kutengana.
Kupitia ukurasa wake wa instagram, mwanadada huyo
alisema: “Nimemvumilia vya kutosha, kuhusiana na tabia zisizokuwa na
nidhamu wala heshima ya ndoa na sasa imefika kikomo.”
Msanii huyo anayemiliki Machozi Band, alibadili
picha ya wasifu ya mtandao huo na kuweka jicho linalotoa machozi na
kidole kikivuja damu.
Alisema kuwa yeye na Gadner hawajaachana kama ambavyo watu wanasema isipokuwa yeye ndiye aliyeamua kumuacha mwanamume huyo.
Hata hivyo, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Gadner alisema: “Sina comment katika hilo.”
Aliongeza kusema: “Aliyezungumza ni mtu mzima na
amefanya juhudi kuzungumza alichozungumza. Ku-comment kwa kupinga au
kukubali ni kuzidharau juhudi zake.”
Meneja wa mwanamuziki huyo maarufu kama Rapa
Wakazi, alisema kuwa kilichozungumzwa na kuandikwa na mwanamuziki huyo
ni kati ya mwimbaji huyo na mashabiki wake, hivyo hakuna cha kuongeza.
Meneja huyo alisema ingawa mwanamuziki huyo
hakuhusisha uongozi wakati anaandika, lakini hayo ni mawazo yake na
yabaki kuwa hivyo.
No comments:
Post a Comment