Dar es Salaam. Serikali imetangaza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inayohuisha na kufuta sera kadhaa zilizosimamia sekta hiyo, huku elimu ya msingi ikitakiwa kuwa ya bure na kuishia kidato cha nne, lakini wadau wa elimu nchini wana shaka kama utekelezaji wake utafanyika kwa ufanisi.
Sera hiyo inaweka msingi wa kutatua matatizo mengi
ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wadau wa elimu kuanzia ufundishaji
hadi maslahi ya walimu, ikitoa matamko ambayo Serikali inatakiwa
iyatekeleze, mengi katika kipindi kifupi.
Katika sera hiyo, kutakuwa na mabadiliko makubwa
kwenye mfumo wa elimu ya awali, msingi na sekondari utakaokuwa wa muundo
wa 1+6+4+2+3+, mfumo ambao utamaanisha kuwa elimu ya msingi ambayo
itaanzia chekechea hadi kidato cha nne, itakuwa ni lazima na ya bure,
badala badala ya unaotumika sasa wa 2+7+4+2+3+, ikimaanisha chekechea ni
miaka miwili, msingi saba, sekondari minne, elimu ya juu ya sekondari
miaka miwili na elimu ya juu miaka mitatu na zaidi.
Katika mabadiliko hayo, umri wa kuanza shule pia utabadilika, sanjari na muda wa elimu msingi ya lazima kuwa miaka kumi.
Mabadiliko mengine ni kujumuishwa kwa mitalaa ya
mafunzo ya ufundi, teknolojia ya habari ili kuwezesha wahitimu kupata au
kuwa na soko nchini au nje.
Pia, sera hiyo imeainisha kuwapo kwa mkinzano
baina yake na Sera ya Ajira na Utumishi wa Umma ya mwaka 1999 inayotamka
kuwa sifa ya kuajiriwa katika utumishi wa umma kwa masharti ya kudumu
ni kiwango cha elimu kisichopungua elimu ya sekondari ya kidato cha nne.
Pia, inaainisha sera hiyo kuwa ushirikiano wa
Tanzania na nchi nyingine kikanda na kimataifa umeleta msukumo wa
kurekebisha Sera ili kuzingatia masuala ya ushirikiano na utangamano.
Masuala hayo ni pamoja na kuoanisha mitalaa; ulinganifu wa viwango vya elimu na mafunzo; upimaji na utoaji tuzo;
Kutokomeza kutojua kusoma na kuandika pamoja na
ulinganifu wa sifa za kujiunga na vyuo vya elimu na mafunzo; na kuleta
ulinganifu wa mifumo ya elimu na sifa za wahitimu kikanda.
Kwa kuwa Tanzania siyo kisiwa, sera hiyo inajikita
katika kuimarisha utangamano katika elimu na mafunzo ili kumjengea
Mtanzania ujuzi, umahiri na uwezo wa kukabiliana na mahitaji
yanayojitokeza katika ulimwengu wa kazi na maisha kwa ujumla.
Inasema sera hiyo mpya kuwa tangu kuanza
kutekelezwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo (1995), Sera ya Elimu ya Ufundi
na Mafunzo (1996) na Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu (1999) kumekuwa na
mabadiliko mbalimbali ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kisayansi na
kiteknolojia ambayo yameleta changamoto na kuzifanya Sera hizo zipitwe
na wakati.
Inaeleza sera hiyo kuwa mabadiliko ya kiuchumi
duniani yamesababisha msukumo kwa nchi zinazoendelea na zilizoendelea
ama kubadilisha au kuimarisha sera, programu na mikakati yake ili ziweze
kuhimili ushindani wa kiuchumi na kuleta maendeleo endelevu ya kijamii,
kisayansi na kiteknolojia.
No comments:
Post a Comment