Dar es Salaam. Kwa mara nyingine Serikali ya Kenya imepiga
marufuku magari yaliyosajiliwa Tanzania kupakia au kushusha watalii
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ya Jomo Kenyatta (JKIA), hifadhi za
taifa na mapori ya akiba nchini humo.
Marufuku hiyo inayoanza leo ilitolewa jana na
Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki, Biashara na Utalii wa Kenya,
Phyllis Kandie alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini
Nairobi.
Uamuzi huo ambao ulitolewa kwa mara ya kwanza
Desemba 2014 na baadaye kubatilishwa, umefikiwa kwa kuwa magari ya Kenya
wanayobeba watalii hayaruhusiwi kuingia kwenye viwanja vya ndege na
hifadhi za taifa za Tanzania.
Waziri huyo alisema kuwa baada ya Kenya kupiga
marufuku Desemba 22 mwaka jana, Waziri wa Maliasili na Utalii wa
Tanzania, Lazaro Nyalandu alikwenda nchini humo na kuomba muda wa wiki
tatu kushughulikia suala hilo.
Walipotafutwa kwa njia ya simu, si Nyalandu, naibu
wake, Mahmoud Mgimwa wala katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Adelhelma Meru
waliopatikana na walipotafutwa kwa simu, hawakupokea.
Waziri kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
Mchungaji Peter Msigwa, alisema Kenya inafanya hivyo kushinikiza
kufunguliwa kwa mpaka wa Bologonja uliopo kati ya nchi hizo mbili.
“Ni hekima tu inayotakiwa itumiwe na serikali
yetu. Wizara inabidi ipime ipi faida na hasara,” alisema Msingwa ambaye
pia ni mbunge wa Iringa Mjini.
No comments:
Post a Comment