Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) imetajwa katika utafiti kuwa ni kati ya taasisi zilizoshika
nafasi za juu kwa kupokea rushwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Utafiti huo unaoitwa ‘Baada ya muongo mmoja wa
kupambana na rushwa, tumepiga hatua kiasi gani?’ umefanywa na Taasisi ya
Afrobarometer ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Repoa na ulifanyika
kati ya Agosti 26 hadi Septemba 29, 2014 kwa kuwahoji watu 2,386 kutoka
Tanzania Bara na Visiwani.
Utafiti huo umeutaja mwaka 2014 kuwa ndiyo
uliokuwa kinara wa matukio ya rushwa katika kipindi cha miaka 10
iliyopita huku asilimia nyingi zikiwataja maofisa wa Takukuru
kujihusisha na vitendo hivyo.
Akizindua matokeo hayo, Mkurugenzi wa Elimu kwa
Umma wa Takukuru, Mary Mosha alisema taasisi hiyo inanyooshewa kidole
kwa kuwa wananchi wanataka kuona kila anayetuhumiwa anafikishwa
mahakamani.
“Mambo yanafanyika lakini hayawafikii watu wa
chini. Walipenda kusikia fulani kapelekwa mahakamani. Watu wanaweza
kusema taasisi fulani kuna rushwa kwa sababu kuna vitu fulani
havijafanyika,” alisema Mosha.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo alisema kama utafiti
huo ungefanyika Oktoba mwaka jana, anaamini matokeo yangekuwa tofauti
kwa namna taasisi hiyo ilivyolishughulikia suala la uchotwaji fedha
kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema baadhi ya watu wanailaumu Takukuru
bila kufikiri kuwa taasisi hiyo haina nguvu ya kisheria ya kutekeleza
mambo inayotaka.
“Pia nendeni kwenye vyama vya siasa chunguzeni
namna wanavyojikusanyia fedha kwa ajili ya uchaguzi, angalieni na sekta
binafsi. Kuondoa rushwa nchini hii inahitajika nguvu ya umma,” alisema
Dk Bana.
Matokeo ya utafiti huo yamebainisha kuwa asilimia 64 ya wananchi waliohojiwa walisema kuwa rushwa inazidi kuongezeka nchini.
Ripoti hiyo iliyotolewa na mtafiti kutoka Repoa,
Rose Aiko inaeleza kuwa asilimia 29 ya wananchi waliohojiwa walisema
kuwa maofisa Takukuru wanapokea rushwa ikiwa ni ongezeko la asilimia
moja ikilinganishwa na matokeo ya utafiti kama huo uliofanywa mwaka
2012.
“Mambo yameongezeka, mwaka 2014 ulivunja rekodi
ingawa kuna hatua zinaonyesha kuchukuliwa lakini hali inaonekana kubaki
vilevile,” alisema Aiko.
Matokeo ya utafiti huo pia yanaonyesha kuwa
asilimia 50 ya waliohojiwa wanasema kuwa Polisi inaongoza kwa kupokea
rushwa nchini wakati maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wanafuatia wakiwa na asilimia 37, majaji na mahakimu asilimia 36, huku
maofisa wa Serikali za Mitaa wakipata asilimia 25.
No comments:
Post a Comment