Saturday, 14 February 2015

BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA KUKUTANA KWA DHARURA ..>>

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linataraji kukutana kwa dharura kesho Jumapili ili kuweka mikakati ya kuimarisha makubaliano ya kusitisha mapigano Mashariki mwa Ukraine yaliyofikiwa mjini Minsk nchini Belarus, wanadiplomasia wamesema.

Wajumbe 15 wa baraza hilo wanajiandaa kupitisha mapendekezo yaliyoandaliwa na Urusi yanayotoa wito kwa pande zote kutekeleza makubaliano hayo ambayo yanatoa makataa ya kusitisha vita kuanzia kesho Jumapili.

Makubaliano yaliyofikiwa na rais wa Urusi Vladimir Putin na viongozi wa Ukraine , Ufaransa na Ujerumani, yameonekana kushindwa huku mapigano makali ya jana Ijumaa yakisababisha vifo vya watu 28.

Mapigano hayo kati ya jeshi la Ukraine na waasi wanaoiunga mkono serikali ya Urusi yanalenga kuudhibiti mji wa Debaltseve, mji unaolezwa kuwa muhimu kwa wapiganaji hao.

Mkataba wa amani ulioafikiwa kati ya Ukraine na Urusi, chini ya wasuluhishi Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francois Hollande unatarajiwa kuanza kutekelezwa leo usiku.

No comments:

Post a Comment