Maelfu ya raia wameandamana katika mji mkuu wa Niger, Niamey, Jumanne wiki hii dhidi ya Boko Haram. Maandamano haya yamefanyika wakati watu 160 wanaoshukiwa kushirikiana na kundi la Boko Haram walikamatwa hivi karibuni nchini Niger
Maelfu ya raia wameingia mitaani ili kuonesha hasira yao dhidi ya ugaidi ambao umekithiri siku za hivi karibuni nchini Niger.
Watu hao waliandamana hadi kwenye eneo kunakopatikana majengo ya Bunge, mjini Niamey, ambapo rais wa Niger, Mahamadou Issoufou, amekua akiwasubiri. Vijana wengi, wanawake, viogozi wa dini mbalimbali, Wakristo na Waislamu wameandamana, huku wakisema: " Jeshi letu ni ufahari kwetu" au " Boko Haram ni Haram (kilichopigwa marufuku)".
Karibu watu 100, 000 wameandamana, huku wakiunga mkono vikosi vya ulinzi na usalama vinavyoendesha vita dhidi ya kundi la Boko Haram, mashariki mwa Niger, katika mkoa wa Diffa na Ziwa Chad. " Hii ni njia yetu ya kupambana dhidi ya uvamizi wa Boko Haram", amethibitisha mmoja kati ya waandamanaji.
No comments:
Post a Comment