Wakati Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeziagiza kampuni za simu kutoa maelezo kuhusu mabadiliko ya gharama za vifurushi vya muda wa maongezi, Vodacom Tanzania imeeleza kuwa mabadiliko hayo yanatokana na ongezeko la kodi na hivyo kulazimika “kubadili mazingira ya kibiashara ili kuepuka hasara”.
Kampuni nyingine kubwa ya mawasiliano, Tigo
imeahidi kutoa ufafanuzi wa suala hilo kesho wakati Airtel imesema
haijafanya mabadiliko yoyote kwenye gharama za vifurushi vyake.
Kumekuwapo na mijadala mingi katika mitandao ya
kijamii kupinga bei mpya za vifurushi hivyo ambazo zimeelezwa kuwa ni
megabati nane kwa vifurushi vyote vya saa 24, na megabati 60 kwa
vifurushi vya wiki.
Bei hizo zinaelezwa kuwa zimeanza kutumika kwa
wateja wanaotumia mitandao ya kampuni za Vodacom na Tigo, ambazo
zinachuana vikali sokoni, huku baadhi ya wateja wa kampuni ambazo
hazifanya mabadiliko ya gharama hizo wakiwashiwishi wenzao kuhama ili
kutokuwa hewani kutokana na kukosa vifurushi.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma
alisema kuwa tayari mazungumzo kati ya mamlaka yake na kampuni hizo za
mawasiliano yameshafanyika na kilichobaki ni wao kutoa maelezo ya hatua
walizoichukua.
“Matumizi ya intaneti yameongezeka nchini na
wananchi wengi wamekuwa hawajui namna ya kutofautisha vifurushi vya muda
wa maongezi na vile vya intaneti. Lakini nimezungumza na kampuni zote
na tumefikia mwafaka. Ndani ya wiki hii watatoa tamko lao pamoja na
msimamo wa bei za vifurushi,” alisema Profesa Nkoma.
Machi, 2013, Profesa Nkoma alisema angehakikisha
kampuni za simu zinawasilisha kwake makubaliano kuhusu punguzo la
gharama za kupiga simu kwa mwingiliano wa mawasiliano, kutoka wateja wa
kampuni moja kwenda nyingine.
Mabadiliko ya gharama na ukubwa wa vifurushi
yalianza kujitokeza mwishoni mwa wiki iliyopita, hali iliyoibua mijadala
mingi katika mitandao ya kijamii. Kilichojitokeza ni kwamba makampuni
hayo yamepunguza ukubwa wa vifurushi vya intaneti na kutoathiri vile vya
muda wa maongezi na ujumbe mfupi hali, iliyozusha hamaki kwa wateja
wengi wanaotaka kujua sababu za mabadiliko hayo.
Baada ya mijadala hiyo kuongezeka, Naibu Waziri wa
Sayansi na Teknolojia, January Makamba aliwaondoa wasiwasi wateja baada
ya kuandika katika ukurasa wake wa facebook kuwa serikali imechukua
hatua mara moja.
“Nimeongea na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa
John Nkoma na nimemuagiza azungumze na kampuni za simu juu ya mabadiliko
ya bei za bundles (vifurushi): ukubwa, ughafla na upamoja (mitandao
yote).
Nimewaagiza pia watoe majibu kwa umma haraka iwezekanavyo. Kampuni za simu hazipaswi kupanga au kuratibu kwa pamoja bei; tukigundua hilo limetokea ni ukiukwaji wa kanuni za ushindani wa soko,” inasema sehemu ya ujumbe huo.
Nimewaagiza pia watoe majibu kwa umma haraka iwezekanavyo. Kampuni za simu hazipaswi kupanga au kuratibu kwa pamoja bei; tukigundua hilo limetokea ni ukiukwaji wa kanuni za ushindani wa soko,” inasema sehemu ya ujumbe huo.
Katika ujumbe wake, Makamba anafafanua kuwa Sheria
ya udhibiti wa mawasiliano haiipi serikali nguvu ya kupanga bei,
isipokuwa gharama za muingiliano
“Inawezekana gharama za uendeshaji, ikiwamo umeme,
zinapanda, lakini hakuna kodi mpya ya Serikali tangu baada ya bajeti.
Huko nyuma ushindani ulishusha bei kwa sababu hakukuwa na bei elekezi.
Bado niko nje ya nchi kwa safari ya kiserikali, lakini nimekuwa
nalifuatilia suala hili kwa karibu. Pia nimeongea na Mkurugenzi Mkuu wa
Vodacom, Rene Meza, kuhusu suala hili leo asubuhi,” aliandika Makamba.
No comments:
Post a Comment