Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damiani Lubuva amesema kwamba, kazi ya uandikishaji wa Daftari la Wapigakura inaendelea vizuri hivyo wananchi wasiwe na hofu.
Pia, aliwataka wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro,
Arusha, Shinyanga, Manyara na Mara kujitokeza kwa wingi kujiandikisha
kwenye daftari hilo Juni 9.
“Nimezunguka mikoa ya Singida na Dodoma zoezi hilo
linaendelea vizuri, sasa nashangaa watu wanasema linasuasua jamani haya
maneno mnayatolea wapi acheni tume ifanye kazi yake,” alisema Lubuva.
Jaji Lubuva alisema kwamba watu wanashindwa kujua
kwamba NEC imefanya uchunguzi wa kutosha kuhusu muda wa uandikishaji wa
daftari hilo na kubaini kwamba muda unatosha kwani ifikapo mwisho wa
Julai na mwanzoni mwa Agosti kazi hiyo itakuwa imemalizika.
Alisema wananchi wajitokeze kwa wingi
kujiandikisha kwenye daftari hilo ili wasije wakakosa haki yao ya msingi
ya kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.
Mchambuzi mwandamizi wa Kompyuta wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC), Joseph Mally alisema wananchi wa mikoa ya Lindi,
Mtwara, Iringa na Njombe wamefanikisha kazi hiyo kwa asilimia 100 kwani
walijitokeza ipasavyo na kuwahimiza wakazi wa Kanda ya Kaskazini kuiga
hilo.
Mally alisema wananchi wa mikoa ya kusini na
Njanda za Juu Kusini walitumia ipasavyo haki yao kwa kujitokeza kwa
wingi kuhakikisha wanajiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera alisema
mafunzo waliyopatiwa watendaji wa wilaya za mkoa huo yatahusisha ujazaji
wa fomu zitakazotumika kwenye uandikishaji huo wa wapiga kura kwa
kutumia BVR.
“BVR ni kifaa cha kisasa kinachoandikisha kwa
kutumia kompyuta na kuchukua alama za vidole, saini na upigaji picha kwa
ubora wa hali ya juu ili kuondoa uwezekano wa wapiga kura kujiandikisha
zaidi ya mara moja,” alisema Dk Bendera.
Alisema watakaoandikishwa ni wananchi wote wenye
umri wa miaka 18 na kuendelea na ambao hawakuwahi kuandikishwa ikiwa ni
pamoja na wale watakaotimiza umri wa miaka 18 ifikapo siku ya uchaguzi
Oktoba mwaka huu.
“Wananchi wa mikoa ya kanda ya kaskazini hususan
wa Mkoa wa Manyara wanatakiwa nao wajitokeze kwa wingi kujiandikisha
kwani kwa kushirikiana na wakurugenzi wa wilaya vifaa vitawafikia wote,”
alisema Mally.
Hata hivyo alisema walikabiliwa na tatizo la
umbali mrefu kutokana na jiografia ya mikoa ya kanda ya kusini na nyanda
za juu kusini kwenye baadhi ya sehemu hivyo kusambaza vifaa kwa zaidi
ya siku moja hadi kufikia maeneo yote.
No comments:
Post a Comment