SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), tayari limemaliza mgogoro wa
mkataba uliokuwa ukimhusisha winga, Ramadhan Singano ‘Messi’ na uongozi
wa klabu yake ya Simba.
Messi alikuwa akidai mkataba wake umechezewa na Simba kwani awali
ulitakiwa kumalizika Julai mwaka huu, lakini uliopo kwa uongozi hivi
sasa unaonyesha unamalizika Julai mwakani.
Hivyo katika kikao walichokiandaa TFF juzi kuzikutanisha pande hizo
mbili, umetoka uamuzi wa kufuta mikataba yote na sasa wametakiwa kuingia
makubaliano mapya kwa ajili ya msimu ujao wa 2015/2016.
Kwenye kikao hicho upande wa Simba uliwakilishwa na Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji, Collin Frisch, Messi yeye alikuwa pamoja na Mwenyekiti wa
Chama cha Wanasoka Tanzania (Sputanza), Mussa Kissoky aliyekuwa
akimtetea.
Upande wa TFF alikuwepo Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Celestine
Mwesigwa, aliyekuwa akizihoji pande zote mbili kwenye kikao hicho
kilichochukua takribani saa mbili (kuanzia saa 6 hadi 8 mchana).
Messi hakuupokea vizuri uamuzi huo kwa kudai kuwa: “Wamesema tukae chini
tufanye makubaliano mapya, mikataba yote haipo, lakini kisheria mimi
niko huru, bado sijajua kama tukishindwa kuelewana na Simba itakuaje,
namuachia Mungu.”
Mara baada ya uamuzi huo wa TFF, yapo maswali magumu ya kujiuliza
kutokana na utata ulioghubika suala hilo na namna lilivyomalizwa, baadhi
ya hayo ni:
Nani aliyefoji mkataba?
TFF imeamua kulimaliza suala hili kwa staili ya kufunika kombe ili
mwanaharamu apite, lakini bado haijaweza kutaja ukweli nani alikuwa ana
haki kwenye hilo.
Uamuzi wa TFF bado haujawaingia akilini wadau wa soka, kwani hawajaeleza nani amefoji mkataba huo kati ya Messi au Simba.
TFF inaogopa nini kumtaja aliyefoji?
Hata kama ni Messi ndiye amefoji mkataba aliokuwa nao au Simba imefanya
hivyo, kwanini TFF inaogopa kumtaja aliyehusika au inamlinda mtu na
kukubali kukumbatia uozo kwenye soka letu?
Katibu TFF alikuwa na uhalali kuwahoji?
Tumeona mambo mbalimbali ya usajili na mikataba ya wachezaji ndani ya
TFF yanapitiwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho
hilo.
Hili suala la Messi linalohusisha mambo ya kisheria, limekuwa tofauti
sana kwani hatujaona chombo hicho kikihusishwa badala yake Katibu wa
TFF, Mwesigwa ndiye aliyelimaliza, lipo la kujiuliza je, ilikuwa ni
halali kwa bosi huyo kushughulikia suala hilo.
Mikataba ya wachezaji iliyoko TFF ni mapambo?
Kwa kawaida mchezaji anapoingia mkataba na timu, taratibu zinazofuata ni
yeye kupewa nakala moja nyingine inabakia kwa timu na ‘copy’ moja
hupelekwa TFF kama uthibitisho, huku takwimu zikiingizwa kwenye mfumo wa
kielektroniki.
Kutokana na uamuzi huo wenye utata uliofanywa kwenye sakata hilo, je,
inamaanisha TFF wameshindwa kufananisha mkataba wa Messi waliokuwa nao
na hiyo inayolalamikiwa au mikataba waliyonayo ipo kama mapambo tu?
TFF inatunga sheria kuzikalia au kutumia?
Bado kuna maswali mengi watu wanajiuliza kama TFF inatunga sheria zake
kuzikalia au kuzitumia wakati wanaamua masuala mbalimbali yanayokiukwa?
Hata wale wanaofoji mikataba au nakala yoyote nao wamewekewa sheria za
kuwabana.
Kwa mujibu wa Kanuni za Nidhamu za TFF toleo la mwaka 2012, Sura ya Tano
inayozungumzia masuala ya kufoji, Ibara ya 61 (1, 2 na 3) inasema: “Mtu
yeyote anayejihusisha na masuala ya soka atakayekutwa na hatia ya
kughushi au kutengeneza nyaraka za kisheria kwa lengo za kuzitumia
atafungiwa pamoja na kupigwa faini.
“Kama ni mchezaji ambaye amehusika, atakumbana na adhabu ya kufungiwa
angalau kutocheza mechi sita. Kama ni kiongozi, wakala wa mchezaji au
wakala wa mechi atafungiwa kutojihusisha na shughuli za mpira kwa
kipindi cha miezi 12.”
Messi yupo huru au mali ya Simba?
Mikataba yote miwili inayodaiwa kuwa na utata imefutwa kwenye kikao
hicho na sasa pande hizo mbili zimeambiwa ziingie makubaliano mapya.
Lakini bado haijajulikana Messi yupo kwenye aina ipi ya usajili hivi
sasa, hapa namaanisha yeye bado ni mali ya Simba licha ya mikataba hiyo
kufutwa au ni mchezaji huru anayeruhusiwa kufanya mazungumzo na timu
nyingine yoyote?
Kama ni mali ya Simba, je, ni kwa mkataba upi? Huu ni utata mwingine iliyouanzisha TFF kama bado hawajaujua.
Kwanini Simba tu masuala haya?
Sakata hili la Messi si la kwanza kutokea kwenye klabu hiyo, msimu wa
2007/2008, kiungo Athuman Idd ‘Chuji’ naye aliingia kwenye mzozo kama
huu na Simba baada ya kumaliza mkataba na kujiunga kwa mahasimu wao
Yanga.
Simba ilimng’ang’ania Chuji ikidai bado ina mkataba naye, lakini mkataba
aliokuwa nao Chuji ulionyesha umemalizika, jambo hilo lilimuathiri
kiungo huyo kwa kukaa nje ya dimba nusu msimu na suala hilo lilipelekwa
kwenye vyombo vya dola na kumalizwa kimya kimya. Je, kwanini mambo haya
yanajirudia Simba?
Mchezaji gani anafuata baada ya Messi?
Udhaifu wa TFF kushindwa kuyaamua masuala haya ya utata kwenye usajili
ambayo yanajirudia kila kukicha, imepelekea wahusika wa mambo hayo
kuendelea kuyafanya kila siku unapofika wakati wa usajili.
Kutokana na historia ya masuala hayo kujirudia, lipo la kujiuliza kwenye
hilo, je, ni mchezaji gani anayefuata kufanyiwa hilo tena baada ya hili
la Messi kumalizwa kienyeji?
No comments:
Post a Comment