Uchunguzi juu ya mwenendo wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa)
katika kashfa nzito za rushwa unaendelea kwa kasi, ambapo polisi wa
Uswisi wamezikamata kompyuta zenye taarifa nyeti juu ya yaliyojiri.
Askari
hao walioanza uchunguzi wa mchakati wa kupata uenyeji wa fainali za
Kombe la Dunia 2018 na 2022 uliotolewa kwa Urusi na Qatar katika
mtiririko huo, waliingia Makao Makuu ya Fifa, Zurich, kuzitaka kompyuta
husika na maofisa wa Fifa wakawakabidhi.
Huko, walifanikiwa
kunakili taarifa zote muhimu, ikiwa ni pamoja na zile za kutoka kwenye
ofisi ya Sepp Blatter, rais aliyechaguliwa tena majuzi kwa muhula wa
tano lakini siku nne baadaye akatangaza kwamba ataachia ngazi.
Taarifa
hizo zinaweza kutoa mwelekeo mzuri wa awali juu ya mambo yatakavyokuwa
kwa uenyeji wa fainali hizo mbili, lakini pia uwezekano wa Blatter,
anayeshikilia urais huo kwa mwaka wa 17 sasa kuhusishwa na rushwa na
hivyo kukamatwa.
Anatarajiwa kuachia ngazi Desemba mwaka huu,
ambapo kuanzia sasa hadi wakati huo, anadai kwamba anasuka mipango ya
mageuzi makubwa katika shirikisho hilo na soka kwa ujumla, ili mrithi
wake acute mipango mizuri mezani.
Hata hivyo, wapo waliotabiri
kwamba huenda akalazimishwa kuondoka ofisini mapema zaidi, kutegemeana
na mwendelezo wa uchunguzi unaofanywa na Uswisi, lakini pia ule wa
Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) ambalo limeshadaka maofisa saba
wa Fifa na wengine saba kutoka nje ya shirikisho hilo.
Wanahusishwa
na tuhuma za wizi wa fedha, rushwa na utakatishaji wa fedha, nyingi
zikiwa na uhusiano na uenyeji wa mashindano au vitendo ambavyo Fifa au
mashirikisho na nchi, waliona inabidi kulipiwa fedha.
Qatar
wanaandamwa zaidi vibaya na matumizi ya hongo kwa wajumbe wa mkutano
mkuu wa Fifa uliowaidhinisha kuwa wenyeji,lakini pia maofisa wa Fifa,
wakiwamo marais au viongozi wa mashirikisho ya soka ya mabara, likiwamo
Afrika – Caf.
Polisi walichukua takwimu kwa njia ya teknolojia ya
habari kutoka kwenye ofisi za Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke na Mkuu
wa Masuala ya Fedha wa Fifa, Markus Kattner. Pamekuwa na madai kutoka
kwa baadhi ya vigogo wa Fifa kwamba wao ndio walioitisha uchunguzi huo,
lakini ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Uswisi inasema kwamba Fifa ndio
majeruhi wenyewe.
Hatua hii imekuja muda mfupi tu baada ya Katibu
Mkuu Valcke kusitisha zabuni kwa ajili ya mchakato wa kupata uenyeji wa
fainali za Kombe la Dunia 2026, akisema ingekuwa upuuzi kuendelea nao
katika mazingira yaliyopo.
Urusi na Qatar zinakana kufanya lolote
nje ya sheria na kanuni kutafuta na kupata uenyeji huo. Haya yanakuja
pamoja na mengine, ambapo Afrika Kusini wanadaiwa kutoa pauni milioni 10
kwa Fifa ili kupata uenyeji wa 2010, ambao ilipata.
Hata hivyo,
Afrika Kusini wanadai kwamba hizo zilikuwa fedha kwa ajili ya kuendeleza
program za soka kwa Waafrika walioko Caribbean. Ufuatilizi wa fedha
hizo unaonesha kwamba ziliingia kwenye akaunti ya Shirikisho la Soka la
Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (Concacaf) na kisha kuchukuliwa
binafsi au kwa mkopo na aliyekuwa mkuu wake, Jack Warner.
Hata
hivyo, Warner aliyedai kwamba Marekani wanaendesha uchunguzi huo kama
kulipa kisasi kwa kukosa uenyeji wa fainali hizo, ameahidi kumwaga
hadharani yote yaliyokuwa yakitokea Fifa, ikiwa ni pamoja na mlungula
uliohusisha maofisa waandamizi.
Jamhuri ya Ireland wanadaiwa
kulipwa euro milioni 10 na Fifa kama kuwaziba mdomo wasifungue kesi
kupinga kukoseshwa kufuzu kwa fainali za 2010 pale Thierry Henry
alipofunga bao akiwa ameshashika mpira na waamuzi wakaliruhusu.
Wakati
hayo yakijiri, kiungo wa zamani wa Brazil, Zico, ambaye majina yake
kamili ni Arthur Antunes Coimbra, 62, ametia nia ya kuwania nafasi ya
Blatter uchaguzi utakapoitishwa Desemba mwaka huu.
Zico ambaye
jina jingine ni ‘Pele Mweupe’ alizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa
habari ulihudhuriwa na waandishi wengi, akasema ni jukumu lake kugombea
ili kuongoza soka na kwamba mzozo wa rushwa ndani ya Fifa umemsikitisha
sana.
“Inasikitisha kwa mchezo wetu huu kuona kinachotokea katika
soka leo – rushwa …na kazi ngumu iliyofanywa na watu wengine wema
imepotezwa bure – hivyo naona ni jukumu langu kutumia uzoefu na elimu
kujaribu kuwania urais,” akasema.
Pamoja na kucheza na kuwa kocha
kwenye nchi mbalimbali sehemu nyingi duniani, Zico ana uzoefu mdogo
katika utawala wa soka katika ngazi ya juu. Anachukuliwa kuwa mmoja wa
wanasoka mahiri katika historia ya Brazil na alicheza fainali tatu za
Kombe la Dunia – 1978, 1982 na 1986.
Nyumbani kwao alitwaa mataji
12 akiwa na klabu ya Flamengo alikocheza tangu 1971 hadi 1983 kisha
akaenda Udinese hadi 1985 akarudi Flemengo kisha akaenda Kashina Antlers
1991 hadi 1994.
Baada ya hapo alijitumbukiza kwenye ukocha, ikiwa
ni pamoja na Japan, CSKA Moscow nchini Urusi na Fenerbahce huko
Uturuki. Kwa sasa anawafundisha FC Goa iliyo Ligi Kuu ya India, akiwa
kocha wake wa kwanza.
No comments:
Post a Comment