MCHEZAJI wa Kimataifa anayechezea klabu ya TP Mazembe ya nchini Congo,
Mbwana Samatta, amemkingia kifua mchezaji mwenzake wa klabu ya Simba,
Ramadhani Singano ‘Messi’ kuwa hana ujanja wa kughushi mkataba.
Mkataba wa miaka miwili wa mchezaji huyo unadaiwa umechezewa kwa
kuongezewa mwaka mmoja zaidi unaoisha Julai, mwakani, tofauti na ule
alionao yeye unaomalizika mwezi ujao.
Akizungumza na MTANZANIA jana akiwa kwenye kambi ya timu ya Taifa ‘Taifa
Stars’, Samatta alisema haamini katika hilo na hafikirii kama Messi
anaweza kuwa na ujanja wa kufanya hivyo, hilo jambo litakuwa limefanyika
ndani ya klabu hiyo.
“Messi hawezi kuwa na ujanja wa kubadilisha mkataba na siamini katika
hilo, siku zote nikiwa kama mchezaji nitasimamia upande wa wachezaji
wenzangu na kwa hilo sikubaliani nalo,” alisema.
Alisema klabu nyingi zimekuwa na ujanja wa kuwabadilishia wachezaji
mikataba, hivyo kuwadhulumu haki yao na hasa mchezaji anapokuwa
anajiandaa kwa makubaliano mapya.
Kwa upande wa Messi, alisema hakuna sehemu yoyote aliyowahi kutamka suala la mkataba wake kughushiwa.
“Mimi nashindwa kuelewa haya mambo, mimi sijawahi kutamka kama mkataba
wangu kughushiwa, mimi nilitaka maelezo kutoka kwa Simba mkataba huu wa
miaka mitatu ni upi,” alisema Messi.
Kauli hiyo ya Messi iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji
Tanzania (Sputanza), Mussa Kisoky, aliyesema Messi hajawahi kutamka
kughushiwa mkataba wake na Simba, bali anachohitaji ni maelezo ya kina
yenye kueleweka.
Kisoky alisema Messi alijaribu kuomba ufafanuzi kutoka kwa viongozi wa
Simba, suala ambalo walishindwa kulifanyia kazi, ndipo alipochukua
maamuzi ya kufika Sputanza.
“Hakuna mahali ambako Messi ametamka kugushiwa mkataba wake, bali
tunachokihitaji ni maelezo ya kina ya kueleweka,” alisema Kisoky.
Mwenyekiti huyo alieleza wamesikia tetesi za Simba kutaka kulifikisha
suala hilo polisi, ila upande wao wanawaonya wekundu hao wa Msimbazi
kutojaribu kuupotosha umma.
“Tumesikia hizo tetesi, lakini kitu cha kujiuliza wanakwenda polisi
kufanya nini, wasipende kudanganya, watambue wanachotakiwa kukifanya ni
kueleza ukweli.
“Suala hili tumeshalifikisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Simba
kutaka kwenda polisi ni maamuzi yao ila watambue tunataka ukweli,”
alisema.
Kisoky alisema wanachotambua tayari TFF wamepokea barua yao ya kuomba kupatiwa ufafanuzi juu ya mvutano huo.
MTANZANIA lilifanya jitihada za kumpata msemaji wa klabu ya Simba, Haji
Manara, ili kutolea ufafanuzi maamuzi ya klabu kulifikisha suala hilo
polisi, hata hivyo simu yake ya mkononi haikuwa hewani.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, alisema tayari barua hiyo imewafikia na wameanza kuifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment