Tanzania tuliamua kuandikisha upya wapigakura katika Daftari la Kudumu baada ya kujiridhisha kuwa tulilonalo halifai. Kutokana na ukweli huo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva aliweka bayana kuwa hataendesha uchaguzi wowote kabla ya uandikishaji kumalizika.
Awali, ilitarajiwa kwamba uandikishaji huo ungekamilika kabla ya Aprili 30, siku iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya upigaji wa Kura ya Maoni lakini mashine za uandikishaji za BVR zilichelewa na kusababisha mchakato huo kusuasua.
Hivi sasa Tume iko katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu na tayari imeshasema utafanyika Oktoba 25. Kama ilivyo kwa Kura ya Maoni, Uchaguzi Mkuu nao utategemea kukamilika kwa uandikishaji huo.
Makadirio yanasema kuwa wanaotarajiwa kuandikishwa ni watu 24 milioni. Kwa siku 96 kuanzia Februari 24 hadi Mei 31, wameandikishwa watu milioni sita tu na kwa mujibu wa ratiba ya Tume uandikishaji unapaswa kukamilika Julai 18, hivyo ndiyo kusema kuwa zimesalia siku 44 tu kuandikisha watu zaidi ya milioni 18.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu la Taifa (NBS), inakadiriwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una wapigakura wapatao milioni 2.9. Hao wanatarajiwa kuandikishwa katika Daftari kwa siku 12 tu kuanzia Julai 4 hadi 16. Sababu inayotolewa na NEC ni kuwa eti mashine zote 8,000 za BVR kwa wakati huo zitakuwa Dar es Salaam jambo ambalo halina uhalisia kwani wakati huo ndipo mikoa ya Morogoro, Pwani na Tanga itakuwa inaendelea na uandikishaji.
Takwimu za NBS zinakadiria kuwa Morogoro ina watu wanaostahili kupiga kura wapatao 1.28 milioni wakati Tanga ina wapigakura wapatao 1.12 milioni. Hao wote kwa ujumla wao ni sawa na watu milioni 2.4 idadi ambayo ni ndogo kuliko ya wapigakura wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini huko wamepewa mwezi mzima wa uandikishaji.
Kwa mtiririko huo wa mambo, hatuoni jinsi ambavyo NEC itakamilisha uandikishaji kabla ya Uchaguzi Mkuu. Hofu hiyo wanayo Watanzania wengi, lakini kama kawaida Tume imekuwa bingwa wa kuweka nta masikioni.
Tunaitaka iongeze kasi ya uandikishaji ili kuwapa matumaini Watanzania hasa kwa sababu uzoefu unatuonyesha kuwa katika maeneo ambayo tayari uandikishaji umekamilika ilibidi ziongezwe siku kwa sababu wapigakura waliojitokeza ni zaidi ya makadirio.
Hivyo, kwa makadirio yasiyo rasmi yawezekana wapigakura wakawa zaidi ya milioni 27. Kama hivyo ndivyo, NEC inabidi ijipange upya na iweke nguvu zaidi kukabiliana na changamoto hiyo, kinyume chake kuandikisha watu zaidi ya milioni 20 kwa siku 44 zilizosalia ni ndoto. Hata kama ikibadili ratiba na kusema itaandikisha mpaka Oktoba 24 bado siku hizo hazitoshi kutokana na mwenendo wenyewe wa uandikishaji unavyoendelea.
Hadi sasa bado malalamiko ya misururu mirefu katika vituo vya uandikishaji yanaendelea sambamba na waandikishaji kuchukua zaidi ya nusu saa kuandikisha mtu mmoja, hali hiyo inadhihirisha kuwa tumefanya makosa kufanya jambo kubwa kama hili la uandikishaji upya wapigakura mwaka wa uchaguzi.
Mambo yamekuwa mengi, tumejizonga na kuzongeka na sasa joto la wasiwasi linazidi kupanda. Ndiyo maana tunasema tunapaswa kutafuta mpango B mapema kabla hatujaenda mrama.
No comments:
Post a Comment