Hamasa na
mapenzi makubwa waliyokuwa nayo Watanzania kwa timu yao ya Taifa, Taifa Stars
yamepotea siku za karibuni kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo matokeo
mabaya ya timu hiyo.
Hilo,
limemfanya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said
Mtanda afikirie kivingine na kutoa ushauri.
Jana,
Mtanda aliyekuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi wa jezi mpya za Stars
alitaka mashabiki na wadau wengine wa soka kurejesha mapenzi yao kwa Taifa
Stars.
Uzinduzi
huo uliofanyika jijini Dar es Salaam ulikwenda sanjari na utoaji vyeti kwa
makundi mbalimbali ya watu, waliotoa mchango wao kwenye maendeleo ya mchezo wa
soka nchini.
Katika
uzinduzi huo, kulizunduliwa jezi aina tatu, ambazo ni jezi za ugenini, jezi za
nyumbani na jezi zitakazokuwa zikitumika kwa ajili ya mazoezi.
Mtanda,
ambaye ni Mbunge wa Mchinga mkoani Lindi alisema uzinduzi wa jezi hizo uwe
chachu ya kurudisha hamasa na mvuto wa timu ya Taifa kwa Watanzania.
Alisema
kuwa anaamini mabadiliko hayo ya jezi yatakwenda sanjari na hatua madhubuti za
kuziimarisha timu mbalimbali za Taifa zifanye vizuri katika mashindano
mbalimbali zitakayoshiriki.
“Kuna
watu wanahoji hivi tunahitaji jezi mpya au timu yetu ya Taifa kufanya vizuri?
Mimi naona tunahitaji vyote viwili. Tubadilishe namna ya kuendeleza timu yetu
ya Taifa pia tubadilishe jezi zinazotumiwa Taifa Star,” alisema Mtanda.
Jezi
hizo zitaanza kutumiwa na Stars kwenye maandalizi yao ya kufuzu fainali za
Mataifa ya Afrika (Afcon) na Michezo ya wachezaji wa ndani (Chan), zitakuwa ni
nyeupe kwa mechi za ugenini, wakati kwa mechi za nyumbani zitakuwa za rangi ya
bluu.
Akizungumza
baada ya uzinduzi huo, kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij alisema kuwa kikosi
chake kiko tayari kwa ajili ya kupeperusha vyema bendera ya nchi katika
mashindano yanayoikabili.
Nooij
alisema kuwa kila mmoja kikosini anatambua deni ambalo timu hiyo inalo kutoka
kwa mamilioni ya Watanzania, hivyo watapambana kuhakikisha wanaibuka na ushindi
kwenye mechi hizo dhidi ya Misri na Uganda.
“Tunaendelea
na maandalizi yetu na molali ya wachezaji iko juu. Wachezaji wanaendelea
kuimarika siku hadi siku na kila mmoja wetu anajituma kwa kadri ya uwezo na
majukumu yake ili tuwape furaha Watanzania,” alisema.
No comments:
Post a Comment