MAISHA haya siku hizi balaa tupu! Mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kwembe, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam (jina limefichwa), anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kituo cha Magomeni kwa madai ya kumchoma kisu dereva wa daladala.
Dereva akiwa miguuni mwa mwanafunzi.
TUJIUNGE ENEO LA TUKIO
“Basi lilikuwa limebeba wanafunzi wengi na abiria wengine, tulipofika eneo la Manzese mtuhumiwa alianza kugombana na mwanafunzi mwenzake wa kike, ugomvi ambao haukujulikana chanzo chake.
“Kifupi waligeuka kero, kondakta wa daladala akaona ili kumaliza vurugu kwenye chombo chake cha usafiri ni vema amshushe mtuhumiwa pale Manzese ili apande gari jingine,” mmoja wa abiria wa gari hilo ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, aliliambia Uwazi.
BAADA YA MTUHUMIWA KUSHUSHWA
Mashuda wa tukio hilo waliendelea kueleza walichokiona, kuwa baada ya mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 14 kushushwa, aligeuka mbogo, akaanza kukodolea macho ardhi, kumbe alikuwa akisaka silaha; akaokota jiwe akiazimia kufanya kile kilichotafsiriwa kama shambulio dhidi ya kondakta aliyemshusha.
Inaelezwa kuwa kitendo hicho kilimchefua dereva; akaona loo! Itakuwaje mwanafunzi huyo akirusha jiwe kwenye gari na kuvunja vioo ilhali yeye ndiye aliyekabidhiwa na mmiliki? Akafunga breki na kumshukia ‘dogo’ huyo kwa lengo la kumdhibiti asilete madhara.
Mwanafunzi anayedaiwa kumchoma kisu dereva huyo.
KILICHOMKUTA DEREVA
Unaweza kusema kwamba hesabu za dereva huyo mrefu, mweusi hazikuwa sahihi, alichokiwaza mwanzo kuwa kingewezekana kirahisi hakikuwezekana. Akashindwa kumtuliza denti huyo ambaye wakati huo alikuwa akisema:
“Mtanishushaje Manzese wakati mimi naenda Magomeni na hapa sina nauli? Sikubali kuonewa, nasema sikubali.”
Naye Omary Juma, mmoja wa abiria waliokuwemo ndani ya daladala hilo, alilieleza Uwazi kuwa mwanzo lilionekana kuwa ni tukio la kawaida, watu waliokuwa eneo hilo na wa kwenye gari walibaki kushuhudia kama ‘kijisinema fulani hivi cha bure’ si unajua tena kuliwaza akili zilizochoshwa na msoto wa maisha!
MWANAFUNZI AZUA TAHARUKI
Ibilisi ni ibilisi tu, hakuna mdogo wala mkubwa. Walichodhani watu kuwa ni kitu kidogo kikakua ghafla, mwanafunzi huyo inadaiwa kuwa alichomoa kisu kutoka maungoni mwake na kumchoma dereva kifuani, akaanguka chini huku akivuja damu, jambo ambalo lilizua taharuki kubwa miongoni mwa mashuhuda.
Kama kawaida, mjini tukio lazima likusanye watu almaarufu ‘nzi’ wa kushuhudia. Kila aliyefika pale alimshuhudia dereva akitapatapa pale chini kutetea uhai wake huku kisu kikiwa kimezama kifuani.
Hapo ndipo wasamaria wema walipomfungia kazi mwanafunzi yule na kumdhibiti asitoroke.
Baada ya udhibiti huo, walimchukua dereva na kumwingiza ndani ya daladala lake tayari kwa safari ya kuelekea polisi kisha hospitali huku kondakta akigeuka ‘suka’ wa muda.
DENTI WA KIKE AIBUKA
Wakati hayo yakiendelea, mwanafunzi wa kike ambaye awali alikuwa na ugomvi na mtuhumiwa, aliibua simanzi nyingine baada ya kuibuka na kudai kuwa majeruhi alazwe magotini mwake (kama picha kubwa iliyopo ukurasa wa mbele inavyoonekana) ili hata akifariki dunia, afie mikononi mwake kwani aliamini alikutwa na mkasa huo akimtetea yeye.
“Yaani wote tulishangaa, yule msichana hakuogopa damu, alimpakata yule dereva huku akibubujikwa na machozi, kiukweli safari iligeuka kuwa ya majonzi,” shuhuda mwingine wa tukio hilo alisema bila kujitaja jina.
UWAZI LAFUATILIA HATIMA YA DEREVA
Baada ya tukio hilo la kusikitisha, Uwazi lilifuatilia hatima ya dereva huyo aliyelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu na kubaini kuwa hali yake ya kiafya ilikuwa ikiendelea vyema ambapo alisimulia tukio zima lilivyokuwa.
“Nilipakia wanafunzi kama 35 pamoja na abiria wengine kutoka Mbezi, tulipofika Manzese niliona ugomvi unazidi kuwa kero kati ya wanafunzi wawili, wa kike na wa kiume, nikaona niingilie kati kutuliza hali ya hewa.
“Kumbe yule mwanafunzi wa kiume alikuwa na kisu, akanichoma kifuani. Nilivuja damu nyingi sana, nikapoteza fahamu lakini namshukuru Mungu naendelea vyema, nawashukuru walionisaidia akiwemo yule mwanafunzi wa kike ambaye naambiwa alikuwa anazuia damu yangu isitoke kwa wingi,” alisema dereva.
MWANDISHI AMCHUNGUZA MTUHUMIWA
Uchunguzi wa mwandishi wa habari hii umebaini kwamba mwanafunzi anayetuhumiwa kutenda kosa hilo, anaishi na baba yake mlezi eneo la Magomeni huku akitajwa kupotezana na baba yake mzazi kwa kipindi kirefu na kukosa mawasiliano naye.
...Akiwa Muhimbili.
POLISI HAWA HAPA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Camilius Wambura amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanamshikilia mwanafunzi huyo kwa mahojiano zaidi. “Tukio likitokea lazima tulichunguze, upelelezi ukikamilika tutamfikisha kwenye vyombo vya sheria,” alisema ACP Wambura.
KUTOKA KWA MHARIRI
Mhariri wa Uwazi analaani kitendo cha watu kujichukulia sheria mikononi na kuwaasa wanafunzi kuacha kufanya hivyo kwa sababu matukio kama hayo ya vurugu yanaweza kuwafanya wakapoteza dira ya maisha yao na kuishia vifungoni.
Aidha, anaviomba vyombo vinavyosimamia masuala ya usafiri kuendelea kutoa elimu kwa wanafunzi na madereva ili kuondoa chuki zinazotokana na uendeshaji wa shughuli za usafiri wa wanafunzi hasa maeneo ya mijini.
No comments:
Post a Comment