MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, amehusishwa na tuhuma za
kutaka kumiliki ardhi kwa njia za kifisadi katika maeneo mbalimbali,
ikiwamo Wilaya ya Rombo mkoani humo.
Kutokana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imemwomba Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuzuia mchakato
wowote haramu utakaofanywa na Gama kuhusu ardhi.
RC Gama, alitajwa bungeni na Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Halima Mdee (Chadema) wakati akiwasilisha maoni ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2015/16
mjini Dodoma jana.
Alisema Gama anashirikiana na kampuni binafsi ya Jun Yu Investment
International, anataka kumiliki ardhi iliyokwishalipiwa fidia ya Sh
milioni 168 na Halmashauri ya Wilaya ya Rombo jambo ambalo ni kinyume
cha sheria.
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe jijni Dar es Salaam, katika hotuba
yake, aliambatanisha vielelezo vinavyomwonyesha Gama kuhusika katika
kampuni hiyo.
Aliwataja wahusika wengine kuwa ni Wang Zhigang raia wa China
anayemiliki hisa 48,000, Feng Hu raia China mwenye hisa 49 na Muyanga
Leonidas Gama ambaye ni mtoto wa Gama anayemiliki hisa 3,000.
“Habari tulizonazo, mkuu wa mkoa anamiliki hisa 20,000 ambapo hisa
10,000 zimefichwa kwa mwanahisa wa kwanza na 10,000 nyingine kwa
mwanahisa wa pili kupitia mkataba wa pili uliofichwa, ambao pia
tumeuambatanisha katika hotuba hii.
“Katika hali ya kushangaza, Halmashauri ya Rombo ambayo iliwekeza fedha
zake Sh milioni 168 haitambuliwi na wala haina hisa hata moja katika
kampuni hiyo,” alisema Mdee.
Alisema kambi ya upinzani ina taarifa za kiintelijensia ambazo
zinaonyesha wawekezaji hao wa kichina walilipa Sh milioni 500 kama fidia
kwa wananchi katika ardhi hiyo ambayo Halmashauri ya Rombo ilishalipa
Sh milioni 168, lakini fedha hizo hazijulikani zilipo.
Mdee, pia alimtaja Gama kutaka kufanya ufisadi katika eneo lililopo
Kilalacha ambalo linagusa Jimbo la Vunjo na Rombo lenye ukubwa wa hekta
2,700.
Akizungumzia suala hilo, Mdee alisema eneo hilo lilikuwa mali ya
ushirika uliokuwa ukifahamika kwa jina la Lokolova, lakini katika siku
za karibuni kigogo huyo wa mkoa amekuwa akilinyemelemea kwa kisingizio
cha uwekezaji.
Alisema Gama yupo nyuma ya mgogoro wa ardhi unaokihusisha kiwanja cha
Mawenzi chenye hati namba C.T 056035 kilichokuwa chini ya miliki ya The
Registered Trustees of Mawenzi Sport Club.
“Kiwanja hiki kilikuwa na hatimiliki ya miaka 33 iliyokwisha mwaka 1974.
Mwaka 1994 kupitia kwa aliyekuwa waziri wa ardhi wakati huo, Edward
Lowassa, alitoa amri ya kutwaa maeneo mbalimbali likiwamo hilo.
“Hali ilikuwa salama kwa wakuu wote wa mikoa waliopita, lakini hali
ilibadilika alipoletwa Gama ambaye amekuwa akitumia ofisi yake
kushinikiza kiwanja husika kikabidhiwe kwa matapeli ambao wametengeneza
nyaraka feki na kuziwasilisha kwa Wakala wa Udhamini na Ufilisi (RITA)
na kujitambulisha kama wadhamini wapya baada ya kukabidhiwa na wadhamini
wa awali.
“Wakati matapeli hawa wanaotambulika kwa majina ya Amratlal N. Pattn na
Hittesh H. Solan wakionyesha kikao cha makabidhiano kilifanyika Januari
5, 2008 mbele ya wadhamini wa awali, Devchad Nathu Shah na Mohamedal
Sharriff, taarifa za uhakika ni kwamba Shah alishafariki dunia tangu
mwaka 1979 wakati Sharriff alifariki mwaka 1998,” alisema Mdee.
Awali akitoa hotuba ya makadirio ya wizara yake kwa mwaka 2015/2016,
Waziri Lukuvi alionya makundi yanayochukua ardhi ya wananchi kwa ajili
ya matumizi mbalimbali kutokulipa fidia kwa mujibu wa sheria.
Alisema watumishi wa sekta ya ardhi, watakaobainika kusababisha kero kwa
wananchi, hususan katika halmashauri nchini, watachukuliwa hatua
ikiwamo kufukuzwa kazi.
No comments:
Post a Comment